Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania na Congo DRC Zapiga Hatua Kubwa Katika Ushirikiano
Oct 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Paschal Dotto-MAELEZO

Tanzania na Congo DRC zimekubaliana kushirikiana katika nyanja mbalimbali zikiwemo zile za biashara, ujenzi wa miundombinu na nyingenezo ambazo zitaleta fursa kwa wananchi wa nchi hizo mbili za kusini mwa Afrika.

Akizungumza baada ya mapokezi ya mgeni wake ambaye ni Rais wa Congo DRC, Mhe. Felix Tshekedi, Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ushirikiano wa Tanzania na Congo DRC ni mkubwa kwa sasa.

“Tanzania na Congo DRC tunashirikiana katika nyanja mbalimbali za uchumi, katika ziara yangu hivi karibuni nchini Congo DRC tulikubaliana na Rais Tshekedi kwenye masuala muhimu ya kukuza ushirikiano wetu ikiwemo fursa za kiuchumi, biashara na uwekezaji pamoja na ulinzi na usalama”, amefafanua Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Congo DRC umepiga hatua kubwa ambapo hivi karibuni Mawaziri wa Tanzania, Congo DRC na Burundi walikutana nchini Marekani kwa lengo la kuomba mkopo wa pamoja ili kujenga Reli ya Kisasa kutokea Kigoma Tanzania, Burundi hadi Congo DRC kwa ajili ya biashara.

Kwa upande wake Rais wa Congo DRC, Mhe Felix Tshekedi amesema kuwa, Tanzania na Congo DRC zimekubaliana kutilia mkazo kwenye masuala ya ulinzi na usalama kwani kuwepo kwa amani ndiyo kunafanya nchi hizo kukamilisha miradi ya ushirika kwa pamoja.

“Tumetilia mkazo zaidi kwenye masuala ya ulinzi na usalama kwani bila usalama ni ngumu miradi ambayo tumekuwa tukiipanga kufanikiwa kwa hiyo suala la usalama ni muhimu sana kwetu”, amebainisha Rais Tshekedi.

Tanzania na Congo DRC zimekubaliana kutekeleza miradi mbalimbali ambayo italeta manufaa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi