Tanzania inaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya madini yatakayoifanya kuwa kituo kikuu cha uuzaji wa madini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ifikapo mwaka 2030, huku ikipanga kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ili kufikia lengo hilo Serikali inaendelea kumalizia ujenzi wa jengo la Tanzanite Exchange Centre (TEC) katika eneo la Mirerani, hatua itakayorahisisha biashara ya madini ya Tanzanite na kuongeza thamani ya madini hayo.
“Mbali na kuwa Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa madini, tunalenga kuongeza uongezaji wa thamani hapa nchini, kuanzisha kiwanda cha kuchenjua madini ifikapo mwaka 2030, na kuondokana na kusafirisha makinikia nje, hatua itakayozalisha ajira na kuchangia uchumi wa taifa,” amesema.

Rais Samia pia ametangaza kuanzishwa kwa Mfuko wa Wakfu wa Madini ili fedha zitakazotokana na madini ziweze kunufaisha vizazi vijavyo ambapo amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa madini sio rasilimali inayoweza kuendelezwa kama kilimo.
" Tumeamua kuchukua hatua hii kwa kutambua kuwa madini sio mahindi kwamba ukiyavuna utatenga mbegu ili uyaoteshe tena. Ukichimba madini kuna mwisho wake. Tunataka vizazi vyetu visikute mashimo bali wakute fedha zitokanazo na madini tunayoyavuna leo" amesisitiza Rais Samia.