Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kuwa Kitovu cha Uchakataji Madini
Aug 21, 2023
Tanzania Kuwa Kitovu cha Uchakataji Madini
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akizungumza na wananchi (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayokwenda sanjari na Kongamano la Wadau wa Chumvi mkoani Lindi leo Agosti 21, 2023
Na Wizara ya Madini

Serikali inaandaa mkakati wa kuwezesha uongezaji thamani madini kwa lengo la kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na madini utakaopelekea Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa wakati akifungua Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayokwenda sanjari na Kongamano la Wadau wa Chumvi Mkoani Lindi leo Agosti 21, 2023

"Serikali inaendelea kuhimiza uongezaji thamani madini nchini ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na madini. Katika kuhakikisha kusudio hilo linafikiwa, nawaomba wawekezaji kuendelea kuwekeza katika viwanda vya uongezaji thamani madini," amesema Dkt. Kiruswa
 
Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini ili kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya nchi, amesema katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya Sera mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji, Viwanda na Biashara nchini.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa akisikiliza maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Tume ya Madini alipotembelea banda hilo kabla hajafungua Maonesho ya Madini na Uwekezaji katika Mkoa wa Lindi. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack.

"Ninapenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wadau wote wakiwemo washirika wetu wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi, napenda pia kuwashukuru washiriki wote mliotoka sehemu mbalimbali mliojumuika na wananchi wa Mkoa wa Lindi hii leo, hakika uwepo wenu unadhihirisha umuhimu wa maonesho haya kwamba sio tu kwa watu wa Lindi bali ni dhamira ya Serikali yetu ambayo ina nia kubwa ya kuendelea kuona Mkoa wa Lindi na mikoa mingine ya Ukanda wa Kusini inafunguliwa kiuchumi," amesema Dkt. Kiruswa

Ameendelea kusema kuwa, Serikali itaendeleza jitihada za kujenga na kuimarisha misingi thabiti ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na ujenzi wa viwanda kama ilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema lengo la maonesho ya madini mkoani humo ni kutangaza fursa na rasilimali mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Madini. Amesema kupitia maonesho hayo wawekezaji wanajionea fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.

Kauli mbiu ya maonesho hayo ni "Wekeza Lindi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Maendeleo ya Jamii". Aidha, maonesho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini waliopo ndani na nje ya nchi, ambayo yanayoendelea hadi Agosti 26 mkoani Lindi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi