Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kutekeleza Sera Nishati ya Jotoardhi
Oct 25, 2024
Tanzania Kutekeleza Sera Nishati ya Jotoardhi
Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Shaibu Hassan Kaduara akizungumza leo Oktoba 25, 2024 wakati akifunga kongamano la kumi la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) Jijini Dar es Salaam.
Na Grace Semfuko - MAELEZO

Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Shaibu Hassan Kaduara amesema Tanzania ipo katika nafasi bora ya kutekeleza sera ambazo zitahakikisha usambazaji sawa wa faida za nishati ya Jotoardhi huku ikilinda mazingira na kuchangia malengo ya mabadiliko ya tabianchi kimataifa.

Ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2024 wakati akifunga kongamano la kumi la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) Jijini Dar es Salaam.

Amesema uwepo wa kongamano hilo umekuwa na faida kubwa kwani majadiliano yake yatasaidia kubadilishana uzoefu katika kuendeleza nishati ya Jotoardhi barani Afrika.

"Kongamano hili limeleta ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zingine katika kuendeleza masuala ya Jotoardhi barani Afrika, sisi Tanzania tupo katika nafasi bora ya kutekeleza sera ambazo zitahakikisha usambazaji sawa wa faida za nishati safi huku tukilinda mazingira yetu," amesema Mhe. Kaduara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba amesema dhamira ya Kampuni hiyo ni kuwezesha kikamilifu matumizi bora ya rasilimali ya Jotoardhi nchini na Afrika kwa ujumla.

Nae Mwakilishi wa Jumuiya ya Jotoardhi barani Afrika, Bi. Wera Rutagarama amesema jumla ya watu 600 wamehudhuria katika kongamano hilo wakiwemo Mawaziri, watoa maamuzi serikalini, mabalozi, wakurugenzi na wafanyakazi wa Kampuni za Jotoardhi kutoka katika nchi 14 zenye Jotoardhi barani Afrika na nchi zingine 26 duniani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi