Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kushiriki Tamasha la Vijana Jijini Sochi, Urusi
Oct 09, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Eliphace Marwa

JUMLA ya Vijana 31 wanatarajia kuiwakilisha Tanzania katika tamasha la dunia la vijana linalotarajia kufanyika Jijini Sochi nchini Urusi  kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 22 Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na ujumbe wa Vijana hao leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhiwa bendera ya Taifa,  Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Erick Shitindi alisema tamasha hilo litakuwa na zaidi ya washiriki ishirini elfu kutoka nchi 150 Duniani kote.

 Shitindi aliwapongeza vijana hao kwa fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika tamasha hilo na kuwaomba kuitumia vyema fursa hiyo kwa ajili ya kuiwakilisha vema na kutangaza uzuri wa nchi viongozi kwa mataifa mbalimbali.

“Tamasha hili litatoa fursa kwenu vijana wa Tanzania na mtakapokuwa huko kuzungumzia mambo mazuri ya Tanzania na hasa kutangaza uzuri wa nchi yetu kwa vijana wa mataifa mengine” alisema Shitindi.

Aidha Shitindi aliwaasa vijana hao kwa kutambua kuwa wanakwenda nchi ya ugenini na hivyo kuwa makini kwa kuwa  watakutana na watu mbalimbali wenye tabia, maadili na itikadi za mlengo tofauti tofauti za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.

“ Kama mnavyofahamu Tanzania inasifika Duniani kote kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu na ni nchi yenye maadili safi, hivyo tunategemea nanyi mtaenda kuonyesha nidhamu ya hali ya juu huko ugenini” aliongeza Katibu Mkuu Shitindi.

Shitindi aliwataka vijana hao kueleza uzuri na mandhari ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Serengeti na bonde la Ngorongoro ambalo ni moja kati ya maajabu saba ya dunia kuwa vipo na ni mali ya Tanzania na si vinginevyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Vijana Bi. Venerose Mtenga kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - ambaye ndiye mkuu wa msafara huo, alimuahidi Shitindi kuwa vijana hao watakuwa mabalozi wazuri kwa Tanzania.

“Lengo la tamasha hilo ni kuwakutanisha vijana kutoka nchi mbalimbali duniani ili kujenga mshikamano, kubadilishana uzoefu kidiplomasia, na uzoefu katika mbinu mbali mbali za maendeleo katika utandawazi”, alisema Venerose Mtenga

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi