Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kushiriki Kombe la Dunia - Mchengerwa
Feb 08, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania inatarajia kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Dunia baada ya kumalizika mashindano ya mwaka huu 2022 yanayofanyika Qatar kutokana na mikakati kabambe ya maandalizi inayoendelea hizi sasa.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Februari 8, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye hafla iliyoandaliwa na ubalozi wa Qatar, kuadhimisha siku ya michezo ya nchi hiyo inayofanyika kila jumanne ya mwezi Februari kila mwaka.

Katika hafla hiyo aliambatana ya Katibu Mkuu wake, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, Saidi Yakubu na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha.

Amesema Tanzania inakusudia kushiriki katika mashindano hayo kutokana na mikakati kabambe iliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya michezo nchi nzima.

“Sisi kama Taifa ni muhimu tukubali ili kufanikisha zoezi hili la kushiriki ni  mashindano makubwa kama haya  lazima kujiandaa  na kuboresha miundombinu ya michezo ambapo kwa sasa tumeshatenga shule 56 nchi nzima kwa ajili ya michezo”. Amefafanua Mhe, Mchengerwa 

Aidha, amesema Serikali inakusudia kujenga viwanja vikubwa vya ndani ambavyo vinajumuisha michezo mbalimbali viwili kwenye mji wa Dar es Salaam na Dodoma pia inatarajia kujenga maeneo makubwa ya burudani matatu 

Amemwomba Balozi wa Qatar, Mhe. Hussain Bin Ahmad Al Homaid kuiomba Serikali ya nchi yake kuisaidia Tanzania kwenye eneo la miundombinu ili kuendelea kuimarisha uhusiano uliojengeka baina ya nchi hizo mbili. 

Amemhakikishia Balozi kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari kuendelea kushirikiana wakati wowote kwenye sekta za michezo, Sanaa na Utamaduni kwa faida ya wananchi wa nchi zote mbili.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Al Homaid ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na nchi yake na kuahidi kuendelea kufanya hivyo.

Pia amesema nchi yake imeitenga siku hii ya michezo ili kuendeleza michezo na kuwafanya wananchi wake kuepukana na magojwa yanayoweza kuzuilika kwa kufanya mazoezi.

Amesema kuwa nchi yake inakwenda kuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za kiarabu kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia.

Katika Hafla hiyo, Mhe. Mchengerwa na Balozi  Al Homaid walipiga mpira wa miguu golini kuashiria ufunguzi rasmi wa siku hiyo huku timu ya ubalozi huo na ile ya watumishi wa Shirika la Ndege la Nchi hiyo walicheza  mechi ya kirafiki na timu ya ubalozi kufungwa mabao 8-2 dhidi ya timu ya Shirika la ndege la Qatar.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi