[caption id="attachment_4852" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani ( wa pili kulia kutoka kulia) akimwongoza Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele kwenye ziara ya kukagua eneo la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji la Stiegler’s Gorge, Rufiji mkoani Pwani.[/caption]
Na Greyson Mwase, Rufiji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani amesema Tanzania inatarajia kupata umeme wa uhakika wa Megawati 5000 ifikapo mwaka 2021, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji.
Dk. Kalemani aliyasema hayo katika ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia kwenye eneo la mradi uliopo Rufiji mkoani Pwani.
[caption id="attachment_4855" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (kushoto) akieleza jambo kwa Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) katika ziara hiyo. Anayesikiliza katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.[/caption] [caption id="attachment_4857" align="aligncenter" width="750"] Kipimo cha kupimia kina cha maji (water gauge) katika sehemu ya mto Rufiji uliopo katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.[/caption]Amesema mradi huo uliopo kwenye eneo la Stiegler’s Gorge lililopo Rufiji mkoani Pwani utaongeza umeme wa kiasi cha Megawati 2100 katika gridi ya Taifa
Dk Kalemani alisema kuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 kutachochea ongezeko la viwanda hivyo kuongezeka kwa fursa za ajira na biashara na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema mradi huo ni moja ya mikakati ya Serikali kuhakikisha nishati inakuwa na mchango mkubwa katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika orodha ya nchi maskini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
[caption id="attachment_4858" align="aligncenter" width="750"] Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele ( wa pili kushoto). Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.[/caption]Alisisitiza kuwa mbali na mradi huo, Serikali imeweka mikakati ya kutumia vyanzo vingine vya nishati kama vile Gesi, Makaa ya Mawe, Jotoardhi, Upepo ili kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa uhakika.
Akielezea mafanikio ya mradi huo mbali na upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk. Kalemani alisema kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa shughuli za uvuvi katika mkoa wa Pwani ni pamoja na kukuza sekta ya Utalii.
Akielezea hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa, Dk. Kalemani alisema baada ya timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia kufanya ziara katika eneo la mradi hatua inayofuatia ni wataalam kukaa vikao mbalimbali kujadili namna bora ya kutekeleza mradi pamoja na kubadilishana uzoefu.
[caption id="attachment_4862" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (wa saba kulia) na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani (wa nane kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia katika ziara hiyo.[/caption]Wakati huohuo, Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele alisema kuwa mradi huo unatekelezeka na kuongeza kuwa Ethiopia ipo tayari kutoa ushirikiano mkubwa kupitia wataalam wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mradi unafanikiwa na kukamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani aliwataka wananchi na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji hususan katika mto Rufiji.