Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Kuiuzia Kenya Gesi Asilia
Oct 10, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Ahmed Sagaff - MAELEZO


Tanzania inatarajiwa kuiuzia gesi asilia Kenya kupitia bomba la kusafirisha gesi hiyo litakaloanzia Dar es Salaam hadi Mombasa nchini Kenya. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaeleza Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto amesema ataendeleza jitihada za ujenzi wa bomba hilo zilizoasisiwa miaka michache iliyopita.


“Kuna mradi wa kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombassa, mradi ambao tumeshasaini makubaliano na Rais Uhuru Kenyatta lakini Rais Ruto ameubeba kuwa ndio mradi wake wa kwanza atakaoanza na Tanzania,” ameeleza Mkuu wa Nchi.


Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 600, litakaloanzia jijini Dar es Salaam litapitia Tanga na kuishia Mombasa nchini Kenya, litasafirisha gesi iliyochimbWa kwenye Kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi huku gesi nyingine ikitokea Mnazi Bay mkoani Mtwara.


Mkataba wa kwanza wa ujenzi wa bomba hilo umesainiwa Mei 2022 ambapo mradi huo unaokadiriwa kugharimu Shilingi trilioni 2.32, unatarajiwa kukuza uchumi wa mataifa yote mawili.


Rais Ruto yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo amewasili jana jioni na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stergomena Tax ambapo leo ameonana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi