Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Bi. Latifa Khamis amesema Tantrade imetoa mafunzo kwa wafanyabiashara 3,556 katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Bi. Latifa amesema hayo leo Machi 13, 2025 wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“TanTrade imeendelea kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa kuwawezesha kushindana katika masoko ya ndani na nje kupitia mafunzo ya biashara.
Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, programu 37 za mafunzo zimeratibiwa, zikihusisha wafanyabiashara 3,556,” amesema Bi. Latifa.
Ametaja mada zilizofundishwa katika mafunzo hayo kuwa ni usimamizi na uendeshaji wa biashara ambayo ilikuwa na washiriki 922; Mbinu za kufikia masoko ya ndani na nje ambayo ilikuwa na washiriki 630; taratibu za kuuza nje na uelewa wa mfumo wa taarifa za biashara ambayo ilikuwa na washiriki 253 pamoja na mafunzo kwa wafanyabiashara wa mipakani iliyokuwa na washiriki 51.
Aidha, ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwa ni pamoja na kuhudumia wafanyabiashara 3,256 kupitia kliniki zilizofanyika katika maonesho na mikutano ya kibiashara.
Vilevile mamlaka hiyo imefanikiwa kutatua changamoto 1,298 kati ya changamoto 1,324 ziliwasilishwa, ambapo changamoto 26 zipo katika hatua za utekelezaji, hususan zinazohusiana na mitaji na vibali vya biashara.