Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanga UWASA Kuanzisha Operesheni ya Kuzuia Mivujo ya Maji Nyumba kwa Nyumba
Jan 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Oscar Assenga, Tanga

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga UWASA) imejipanga kuanzisha operesheni ya kuzuia mivujo ya maji nyumba kwa nyumba ili kuweza kuondokana na upotevu wa maji yanayopotea kutokana na uwepo wa hali hiyo.

Hayo yalisemwa leo na Meneja Ufundi wa Tanga UWASA, Mhandisi Rashid Shabani wakati akiwasilisha wasilisho kuhusu kujenga uelewa kuhusu udhibiti wa maji yanayopotea.


Wasilisho hilo aliliwasilisha katika semina kwa wateja wa Jiji la Tanga kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa mkataba wa Huduma kwa Mteja.

Pia, waliitumia kuwajengea uelewa kudhibiti maji safi yanayopotea iliyofanyika Ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo eneo la Mwakidila Jijini Tanga.


Alisema operesheni hiyo itakuwa ni mwarobaini wa kuhakikisha maji yanayopotea yanadhibitiwa na hatimaye kuondokana na tatizo hilo ambalo wakati mwingine limekuwa likiwasababishia hasara.

“Tutaanzisha operesheni zuia mivujo ya maji nyumba kwa nyumba kwa kuangalia mazingira na hilo litatusaidia kuweza kupunguza tatizo la upotevu wa maji”, alisema Mhandisi Shabani.

Hata hivyo alisema pia wataunda kikosi kazi cha kufuatilia wezi wa maji majumbani ambao wamekuwa wakishirikiana na wafanyakazi wao ambao sio waaminifu.

Awali, akizungumza wakati akifungua semina hiyo, Mkurugenzi wa Tanga UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly alisema wanapenda wananchi waelewe njia mbalimbali ambazo maji yanapotea na namna gani kama wananchi wanaweza kusaidia kuokoa maji yanayopotea ili huduma ziweze kuwa endelevu.

Alisema suala la pili kuna mkataba wa huduma kwa mteja ambapo mwaka jana walikutana na baadhi yao kujadiliana suala hilo, alisema kwa sasa mkataba huo umepatikana na wanapaswa kuuelewa mkataba huo.

Alisema kwani viongozi ni watu wa kwanza kuweza kupata fursa ya kupata uelewa na mkataba huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi