Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAMISEMI, PS3 Watoa Mafunzo kwa Wahasibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini.
Jun 04, 2018
Na Msemaji Mkuu

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bibi Rehema Madenge akisisitiza jambo kwa Waweka Hazina na Wahasibu kutoka mikoa ya Dodoma na Singida (hawapo pichani)  leo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi  wa mafunzo ya mfumo wa Epicor 10.2 ambao umeboreshwa na unatarajia kutumika na Halmashauri zote nchini kuanzia Julai 1 mwaka huu.

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.

 Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) wanatoa mafunzo ya kina ya wiki tatu kwa watumishi wa kada  ya uhasibu kutoka  mamlaka  185  za Serikali za Mitaa Tanzania.

Akifungua mafunzo hayo yanayohusu mfumo  mpya wa Epicor 10.2, leo Jijini Dodoma   Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bibi. Rehema Madenge amesema mafunzo hayo ya mfumo wa Epicor yamelenga kuwapa uelewa Wahasibu juu ya mabadiliko ya maboresho makubwa yaliyofanywa katika mfumo huo.

“Historia inaonesha kuwa Halmashauri zetu zilianza matumizi ya mfumo katika toleo lililojulikana kama Platnum mwaka 1999/2000 na baadaye mfumo ulifanyiwa maboresho na kufungwa epicor toleo Na 7.2 mwaka 2001 wakati huo mfumo ukiwa umefungwa katika Halmashauri 38 tu.” Anasema Bibi. Rehema Madenge

 Msimamizi wa Mifumo ya Fedha Ofisi ya Rais TAMISEMI, Augustino Manda akitoa maelezo juu ya lengo la mafunzo ya Epicor 10.2 kwa Waweka Hazina na Wahasibu kutoka mikoa ya Dodoma na Singida (hawapo pichani) leo, Jijini Dodoma.

Anaongeza kwa kufafanua kuwa mwaka 2014/15 mfumo uliboreshwa na kuwa epicor toleo la 7.3.5 na kufungwa katika Halmashauri 44 zaidi hivyo kuwa na Jumla ya Halmashauri 82 zilizokuwa zinatumia mfumo, Rehema Madenge.

Katibu Tawala Bibi. Rehema anazidi kueleza kuwa , Julai Mwaka 2012, TAMISEMI ilifanya maboresho makubwa kwa kuunganisha Halmashauri  133 zilizokuwepo wakati huo kupitia  kampuni ya simu ya taifa TTCL na kuweka epicor toleo namba 9.05 ambalo limeendelea kutumika hadi sasa. Hata hivyo Halmashauri zilizoongezeka baadaye zilifungwa epicor toleo namba 10.1 ambalo limeboreshwa sasa na kuwa 10.2 inayofungwa Halmashauri zote.

Aidha amesema, matumizi ya epicor toleo namba 10.2 ni hatua kubwa sana katika utekelezaji wa dhana nzima ya uwazi uwajibikaji na utawala bora katika usimamizi wa fedha za umma. Hata hivyo amesema, mfumo huo utasaidia Halmashauri kuondokana na vyeti vya hati chafu na zile zenye mashaka kutokana na mapato na matumizi ya fedha zote kutakiwa kuingizwa katika mfumo huo.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mifumo ya Fedha Ofisi ya Rais TAMISEMI Augustino Manda amesema uboreshaji wa mfumo wa Epicor ni muendelezo wa uboreshaji wa mifumo ya Serikali kama ilivyofanyika kwa mifumo mingine kama vile mifumo ya Afya.

Maboresho mengine yaliyofanyika katika mfumo huo wa Epicor 10.2  ni kwamba mifumo yote ya msingi ya usimamizi wa fedha katika sekta za umma kwa sasa itaweza kuwasiliana na kushirikishana taarifa ambapo hapo awali, uongozi na maafisa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa walilazimika kupitia mipango na bajeti katika mfumo mmoja, mapato katika mfumo mwingine na matumizi kwenye mfumo mwingine, hivyo kuleta ugumu katika kudhihirisha uwajibikaji, ufanisi na thamani ya fedha katika matumizi ya fedha za Serikali. Vile vile utaunganishwa na mfumo unaowezesha mabenki kulipana Tanzania (TISS) ambao utaruhusu malipo yote kufanyika kwa njia ya kielektroniki.

Mafunzo hayo yanafanyika katika vituo sita  ambavyo ni Dodoma, Mwanza, Mtwara, Iringa, Kagera na Mbeya yakijumuisha watumiaji wa mfumo huo ambao ni Waweka Hazina na Wahasibu na baadaye Maafisa TEHAMA, Maafisa Manunuzi na Wakaguzi wa Ndani.

Washiriki wa Mafunzo ya Epicor 10.2 ambao ni Waweka Hazina na Wahasibu kutoka mikoa ya Dodoma na Singida wakifuatilia hotuba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Rehema Madenge wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, leo Jijini Dodoma.

( Picha na PS3 )

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi