Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa Laja na Kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
Sep 10, 2024
Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa Laja na Kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika mkoani Ruvuma kuanzia Septemba 20 hadi 23, 2024. Litafunguliwa na Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na kufungwa na Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amesema kuwa Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa linalotarajiwa kufanyika mkoani Ruvuma, litakuwa na vionjo vya kipekee na mahsusi ikiwemo Kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Vionjo vingine vitakavyokuwepo katika tamasha hilo lililobebwa na kaulimbiu ya “Utamaduni wetu ni utu Wetu, Tuuenzi na Kuuendeleza. Kazi iendelee”, ni mirindimo ya kiasili ikijumuisha mavazi, maonesho, visasili na visakale, mdahalo wa kitaifa, onesho maalumu la matumizi ya kanga pamoja na mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania bara na visiwani.

Msigwa ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 23, Septemba 2024 ambalo litafunguliwa na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na kufungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

”Tangu Mhe. Rais aelekeze kufanyika kwa tamasha hili kila mkoa, kumekuwa na mwitiko chanya kwa jamii ambapo kwa mwaka 2022 lilifanyika mkoani Dar es salaam na kuhudhuriwa na washiriki 16,500, mwaka 2023 lilifanyika mkoani Njombe likiwa na washiriki 17,123 na sasa ni mkoani Ruvuma na linatarajiwa kutia fora kwa kuwa na washiriki maradufu ukilinganisha na matamasha yaliyotangulia kutokana na maandalizi yake ya kipekee yanayovutia na yaliyosheeni uanuai wa kiutamaduni”, amesema Msigwa.

Ameyataja madhumuni ya tamasha hilo kuwa ni pamoja na kukuza sekta za ubunifu na utamaduni; kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni; kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa; kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa pamoja na kutangaza fursa na rasilimali za kipekee za nchi.

Ameeleza kuwa, tamasha hilo limekuwa na faida nyingi kwa jamii ambazo ni pamoja na kuenzi utamaduni wa taifa; kuimarisha utangamano wa kitaifa; kuitangaza nchi; kutangaza vivutio vya kiutalii na kiutamaduni; fursa za kiuchumi, kiutamaduni na kijamii pamoja na kutanua wigo na mitandao ya kibiashara kwa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani bidhaa za utamaduni, sanaa, na ubunifu.

Ametoa rai kwa wananchi kushiriki tamasha hilo na kuyaomba makampuni, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kujitokeza kudhamini tamasha hilo kwa kuwa watapata fursa ya kuonesha shughuli zao mbalimbali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi