Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAGCO, SAUT Yawajengea Uwezo Maafisa Habari Kuboresha Mawasiliano Kidijitali
Oct 06, 2023
TAGCO, SAUT Yawajengea Uwezo Maafisa Habari Kuboresha Mawasiliano Kidijitali
Sitta Peter kutoka VETA akipokea cheti kutoka kwa Dkt. Peter Mataba, Mkuu wa idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa umma wakati wa ufungaji wa Mafunzo ya Uboreshaji Mawasiliano Kidijitali kwa Maafisa Habari Serikalini yaliyofanyika kwa siku tano, kuanzia tarehe 2 hadi 6 Oktoba, 2023 katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), jijini Mwanza
Na Mwandishi Wetu

Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Augustino (SAUT) kwa kushirikiana na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) wameendesha Mafunzo ya Uboreshaji Mawasiliano Kidigitali kwa Maafisa Habari Serikalini ili kuboresha ufanisi wa maafisa hao katika utendaji na usambazaji habari sambamba na maendeleo ya teknolojia.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tano, kuanzia tarehe 2 hadi 6 Oktoba, 2023 katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), jijini Mwanza yaliwahusisha maafisa habari 21 kutoka Taasisi, Mamlaka, na Wakala za Serikali.

Akizungumza kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo, tarehe 6 Oktoba, 2023, Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, SAUT, Dkt. Peter Mataba amesema mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa habari ni muhimu ili kuboresha uwezo na utendaji wa maafisa habari Serikalini kwa kuwa teknolojia inaendelea kubadilika.

“Kuna changamoto nyingi zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia katika tasnia ya habari, ili kukabiliana na changamoto hizo, suluhisho ni mafunzo; Msije mkajikuta wanahabari mko nyuma kuliko mnaowahabarisha,” Amesema.

Aidha, amewaomba maafisa hao kuendelea kukishirikisha Chuo na wakufunzi wake juu ya maeneo yenye changamoto katika utendaji kazi wao ili kuwasaidia kubuni mafunzo yenye kutatua changamoto husika.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAGCO, Bw. Abdul Njaidi, aliwataka washiriki wa mafunzo kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Serikali mara kwa mara.

Alisisitiza umuhimu wa maafisa mawasiliano kuwa na ujuzi wa kidigitali ili kuweza kushughulikia majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kuchangia katika kukuza utendaji wa Serikali.

Awali wakati akifungua Mafunzo hayo, Naibu Makamu Mkuu wa SAUT, Profesa Hosea Rwegoshora, tarehe3 Oktoba 2023, aliipongeza TAGCO kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo maafisa habari.

Prof. Rwegoshora Aliwahimiza washiriki kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia yanayotokea kwa kasi na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mafunzo hayo ya kidigitali yalikuwa na lengo la kuwajengea washiriki uwezo katika matumizi ya teknolojia za mawasiliano, kama vile mitandao ya kijamii, mifumo ya kielektroniki, na zana za kidijitali kwa ajili ya kusambaza habari na kuwasiliana na umma ambapo washiriki walipata fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za mawasiliano ya Serikali na jinsi ya kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Mada zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Uandaaji wa Video, Stadi za Uongozi na Usimamizi, Uandaaji na Uwasilishaji wa Hotuba, Usanifu Habari, Uandikaji Muhtasari wa Vikao.

Mafunzo hayo pia yalijumuisha usanifu wa habari, ambao ni muhimu kwa maafisa habari katika kusimamia na kusambaza habari za Serikali kwa umma. Washiriki walipata mafunzo juu ya jinsi ya kukusanya, kuchambua, na kusawazisha habari muhimu ili kufikisha ujumbe sahihi kwa umma kwa njia inayoeleweka na kuvutia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi