Imeelezwa kuwa tafiti zina mchango mkubwa kwa Mabadiliko ya Tabia Jamii katika kuzingatia Kanuni za Afya na kuwa na jamii yenye mwitikio chanya katika kupambana na adui maradhi.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Tumaini Haonga, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma katika kikao cha kujadili na kupokea Matokeo ya Utafiti wa Mabadiliko ya Jamii kuhusu Masuala ya Afya uliofanywa kupitia Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR) ambao uliangazia mwitikio wa jamii kuhusu Masuala ya Afua za Afya Kinga.
Dkt. Haonga amesema kutokana na matokeo ya utafiti huo, jamii imeendelea kuwa na mwitikio chanya huku kukiwa na baadhi ya changamoto kwenye jamii ikiwemo mila potofu, mitazamo tofauti na wananchi kuwa na uelewa tofauti hivyo ni muhimu kuongeza nguvu katika kuwafikia wananchi kwa kuwapa elimu na kuisikiliza jamii inataka nini ili kutoa mwongozo na kuwapa elimu sahihi.
“Tumepata fursa ya kuona matokeo ya utafiti huu ambao kwa sehemu kubwa unaonesha kuwa jamii imekuwa na mwitikio chanya lakini kuna vile ambavyo vimetajwa kuwa ni vikwazo ambavyo vinachangia kutokufikia malengo yakiwemo kuhamasisha wananchi kuwahi vituo vya kutolea huduma za afya, hapa yamehusianishwa ya mila potofu, mitazamo tofauti ya jamii, wananchi kuwa na uelewa tofauti kuhusu kile kinachozungumzwa kabla ya kupewa ufafanuzi, na matokeo haya yanatuambia ni muhimu kuzidisha nguvu katika kuwafikia wananchi kwa kuwapa elimu na tuwe na utaratibu wa kusikiliza jamii ina mtazamo upi kwa afua ambazo tunazipeleka kwenye jamii ili iwe sehemu ya utatuzi“, amesema Dkt. Haonga.
Aidha, Dkt. Haonga amesema Elimu ya Afya kwa Umma inategemea Ushahidi wa Kisayansi unatokana na utafiti kwani ni muhimu na husaidia kutoa mwanga namna nzuri ya kuzingatia kanuni za afya huku akiziomba Taasisi za Utafiti kuongeza nguvu katika suala la utafiti kwenye suala la afya jamii.
“Wito wangu ni kuziomba Taasisi za Utafiti kuweka nguvu suala la afya jamii ili tuweze kufahamu kuwa jamii halisi inahitaji nini maana huwezi kulinganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine”, amesema.
Kwa upande wake Dkt. George Playgod, Mwakilishi kutoka NIMR amesema lengo la kikao hicho ni kujadili ili kuhakikisha wanashirikisha jamii kwa kuwatumia Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii ambapo pia amesema utafiti huo umefanyika katika vipindi mbalimbali vya Ugonjwa wa UVIKO-19.
Ikumbukwe kuwa, kikao hicho kimekutanisha wataalam kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais,-TAMISEMI, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Waratibu na Wawakilishi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Mikoa ya Kigoma, Pwani na Dar Es Salaam pamoja na Chuo Kikuu cha London School of Hygiene &Tropical Medicine.