Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAFIRI Yatakiwa Kufanya Tafiti Zenye Tija kwa Wavuvi Wadogo
Aug 11, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na. Edward Kondela

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetakiwa kujikita kwenye tafiti zenye tija kwa wavuvi wadogo na kushauri vyema kwenye mamlaka za Serikali juu ya njia mbalimbali zikiwemo za kiteknolojia ili sekta ya uvuvi iwe na tija zaidi kwa mvuvi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo kujionea namna taasisi hiyo inavyofanya kazi na baadae alishuhudia maendeleo ya ukarabati wa majengo ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Akiwa katika ofisi za TAFIRI zilizopo Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Ulega amefafanua kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo ni lazima zijibu changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo hivyo ni muhimu kufikiria mambo ya kufanywa ili kuondoa changamoto hizo ikiwemo ya zana za uvuvi kutokana na mazingira ya sasa.

“Nyie ni wataalam wasomi lakini msiache kuwashirikisha na kuwasikiliza wavuvi ambao wamekuwa wakishinda baharini muda mrefu zaidi, mna mambo ya kujifunza kutoka kwao ili kuhakikisha mnawawekea mazingira bora ya kufanyia shughuli zao, ikiwemo kuhakikisha hawavui samaki kwa kuvizia bali wawe wanaelekezwa maeneo yenye samaki kwa kutumia teknolojia ya kisasa.” Amesema Mhe. Ulega

Aidha, ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ongezeko la watu na mahitahi ya samaki, TAFIRI inapaswa kufikiria kwa kina zaidi kwa kufanya tafiti nyingi zaidi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (ZAFIRI), namna ya kuhakikisha wananchi wa Tanzania hususan wadau wa sekta ya uvuvi wananufaika kupitia tafiti zenye matokeo chanya kwao.

Amesema ubunifu pekee ndiyo unaweza kuifanya TAFIRI kuwa karibu zaidi na wavuvi kwa kuwa watakuwa wanapata mafanikio kupitia uvuvi kwa tafiti ambazo zitawapatia zana sahihi za uvuvi kulingana na mazingira ya sasa pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa kufahamu maeneo yenye samaki badala ya kuvua samaki kwa kuvizia maeneo ambayo hawana taarifa za uhakika juu ya uwepo wa samaki pamoja na majira yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei amemuarifu Mhe. Ulega kuwa taaisisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha hali inayosababisha kushindwa kufikia baadhi ya malengo waliyojiwekea katika tafiti kutokana na ukosefu wa vifaa vikiwemo vya maabara.

Pia, Dkt. Kimirei amesema licha ya changamoto hizo TAFIRI imekuwa ikiendelea kuhakikisha inafanya tafiti ambazo ni muhimu kwa sekta ya uvuvi ili kuwa na taarifa sahihi juu ya sekta hiyo ili taifa liwe na dira ya kufahamu rasilimali za uvuvi zilizopo katika Bahari ya Hindi pamoja na maziwa yaliyopo hapa nchini na kufahamu njia sahihi za kutunza rasilimali hizo na pia kuhakikisha zinawanufaisha wavuvi.

Nao baadhi ya watumishi wa TAFIRI wamemuomba Naibu Waziri Ulega, kuwasaidia kupatikana kwa meli maalum kwa ajili ya utafiti kwa kuwa wanashindwa kwenda baharini kufanya tafiti kutokana na ukosefu wa meli ya aina hiyo, jambo ambalo Mhe. Ulega amesema atalifanyia kazi ili taasisi hiyo iweze kupata meli na kufanya tafiti mara kwa mara, pamoja na kupata magari ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi hiyo.

Akiwa katika ofisi za Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) zilizopo Wilaya ya Kigamboni, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amelitaka shirika hilo wakati likiwa katika hatua mbalimbali za kufufuliwa lijipange kibiashara pamoja na kiubia na makampuni binafsi ya uwekezaji.

Mhe. Ulega amesema TAFICO iwe na mkakati na mbinu za kujielekeza zaidi katika uchumi wa bluu ili nchi ifaidike na rasilimali samaki na mazao yake na kuhakikisha uchumi wa wavuvi wadogo unakua ili shirika hilo liwe na tija zaidi.

Mhe. Ulega amemuelekeza Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Prof. Yunus Mgaya kusimamia mbinu na mkakati imara wa ufufuaji wa shirika na kumpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa Prof. Mgaya ana uzoefu mkubwa kwenye sekta ya uvuvi na kwamba ataweka dira imara ya TAFICO katika mikakati ya kuhakikisha shirika linakuwa na tija kwenye sekta ya uvuvi hususan katika uvuvi wa bahari kuu.

“Hivi karibuni haitazidi miezi mitatu tunapokea meli ya uvuvi tunataka ikifika ianze kazi mara moja, meli ikute tumekaa kwenye mpango kazi iende kuvua samaki wa kutosha bahari kuu na ilete hao samaki kwa wingi wauzwe ndani na nje ya nchi.” Amefafanua Mhe. Ulega

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa TAFICO, Bi. Esther Mndeme amesema ukarabati unaendelea kufanywa katika miundombinu mbalimbali iliyopo kwenye eneo hilo baada ya serikali kufufua shirika hilo na kwamba baadhi ya miundombinu inahitaji ukarabati mkubwa na mingine kidogo kutokana na miundombinu hiyo kutofanya kazi kwa takriban miaka ishirini.

Bi. Mndeme amesema licha ya changamoto za kifedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ukarabati huo unafanyika kwa muda uliopangwa ili shirika lianze majukumu yake rasmi kama ambavyo imekusudiwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO, Prof. Yunus Mgaya, amesema shirika likianza kufanya kazi vizuri litaleta tija katika uchumi wa bluu kwa kuwa fursa nyingi zitafunguka na taifa kupata tija zaidi kiuchumi na wavuvi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Fatma Nyangasa amesema uwepo wa TAFICO katika wilaya hiyo kutaongeza chachu ya maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa upande wa ajira pamoja na kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Dar es Salaam kwa kujionea utendaji kazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na ukarabati wa majengo ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi