Na Mwandishi wetu,
Katika kuhakikisha Watanzania wengi wanaongeza hamasa ya unywaji wa maziwa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeunga mkono juhudi za Serikali na Bodi ya Maziwa (TDB) nchini kwa kutoa vifaa vitakavyotumika katika Kampeni ya Kitaifa ya Unywaji Maziwa inayotarajia kufanyika Kitaifa mkoani Kagera kuanzia Mei 28 – Juni 1 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika katika Ofisi za TADB jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga amesema kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeunga mkono Kampeni hiyo kwa kutambua umuhimu wa kuchagiza unywaji wa maziwa nchini kama inavyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani WHO.
“Kwa kutambua umuhimu wa Kampeni hii, TADB kwa kushirikiana na TDB na wadau wengi tumeazimia kuhamasisha unywaji wa maziwa ili kufikia viwango vya kimataifa ya unywaji wa maziwa ambao unakadiriwa kufikia walau lita 200 kwa mwaka kutoka 47 za sasa,” alisema.
Aliongeza kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa TADB ilijumuisha mnyororo wa thamani ya Ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa kuwa ni miongoni mwa minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani wa mifugo nchini.
Akasisitiza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa ili kuchagiza juhudi mbalimbali za Serikali katika ustawi wa sekta ya maziwa hapa nchini.
“Benki inatoa mikopo na kusaidia uwekezaji kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya kuhudumia ng’ombe ikiwemo majosho na mabwawa ya kunyweshea na pamoja na usindikaji wa maziwa kwa ajili ya kuongeza thamani ya maziwa,” alisema Bw. Assenga.
Kwa upande wake Kaimu Msajili wa TDB, Dkt. Mayasa Simba amesema kuwa Kampeni hiyo ya kitaifa yenye kaulimbiu ya ‘Okoa Jahazi, Jenga Afya, Jenga Uchumi kupitia Maziwa’ imelenga kuchagiza dhamira ya Bodi ya Maziwa katika kusimamia, kuratibu na kutoa huduma bora ya ushauri kwa wadau ili kukuza na kuendeleza tasnia ya maziwa iliyo endelevu na yenye ushindani nchini.
“Lengo la Kampeni hii ni kuhamasisha unywaji wa maziwa ili kuhakikisha Watanzania wengi wanafikia viwango vya kimataifa na pia ili kutimiza lengo la Bodi katika kuhakikisha kuwa sekta ya maziwa inayosimamiwa na kuratibiwa vizuri, yenye ushindani kwa lengo la kuboresha maisha ya watanzania na kuongeza mchango wa sekta ya maziwa katika uchumi wa Taifa,” alisema.
Bodi ya Maziwa imeundwa kwa Sheria ya sekta ya Maziwa Sura (262) ambayo iko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yenye jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta hiyo. Bodi ina jukumu la kuhamasisha na kuwawezesha wadau katika shughuli za uzalishaji, ukusanyaji maziwa, usindikaji, kuboresha masoko na unywaji wa maziwa na bidhaa zake.