Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tabora Yajiweka Tayari Fursa Bomba la Mafuta
Aug 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Mwandishi Wetu - MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri amesema kipaumbele cha uongozi wa mkoa wake ni kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa vijana na wananchi wa mkoa huo kuchangamkia kila fursa zitakazotajitokeza Mkoani humo wakati wa ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi mkoa wa Tanga.

“Tunataka tuwaelimishe na kuwahamasisha vijana, kinamama na wananchi wote wa mkoa wetu kuhakikisha wanazitumia fursa zote zitakazojitokana na mradi huu ili waweze kujiendeleza” alisema Mwanri na kuongeza kuwa uongozi wa mkoa wake hauko tayari kuona vijana wanabaki kuwa watu wa kupiga makofi na kushangilia tu.

Mkuu wa Mkoa Tabora alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu katika kijiji cha Chongolieni Mkoani Tanga mara baada ya kuhudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo uliofanywa kwa pamoja na Marais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni na Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Aliongeza kuwa jambo muhimu watakalolifanya ni kuhakikisha kuwa vijana wa Mkoani wa Tabora wanashirikiana kikamilifu na wataalamu ambao watakuwa wakijenga miundombinu ya mradi huo pamoja na kutoa huduma zitakazohitajika ili waweze kufaidika na fursa hiyo za mrai huo.

“Tunauangalia mradi huu kuwa ni fursa nyingine ya kipekee ya kuzidi kuufungua mkoa wetu kiuchumi kwa kuzidi kujenga mazingira mazuri ya kuvutia biashara na uwekezaji”, alisisitiza Mkuu wa Mkoa huyo.

Alifafanua kuwa uwekezaji kwa kawaida una sura nyingi unaweza kuleta mitaji, tekinolojia, kuongeza ajira na kuongeza mapato ya Serikali.

Bwana Mwanri alieleza kuwa kwa uongozi na wananchi wa Tabora wanaona fahari kwa jambo kubwa kama hilo la kihistoria linafanyika katika Mkoa wao ambao bomba hilo litapitia katika Wilaya za Igunga na Nzega.

“Sisi tumejipanga kunufaika vizuri na mradi huu….si ni wakulima wa mpunga, maharage, viazi vitamu, maboga, tikiti maji nk... hizi zote ni fursa zaidi kuinua biashara ya mkoa wetu”, alisema.

Aliongeza kuwa kusema kuwa “Mkoa unazidi kufunguka kwa kasi. Reli ya standard gauge inapita Tabora kwa kilomita nyingi, ukienda Shinyanga, Mwanza, Itigi ukitaka kwenda Kigoma tuko na barabara zetu nazo zinajengwa kuufungua mkoa”.

Mkuu wa Mkoa huyo wa Tabora alifafanua kuwa ulinzi wa bomba hilo utapewa kipaumbele katika mkoa wake na kubainisha kuwa wananchi ndio wakataokuwa walinzi wa awali wa bomba hilo kwa kuwa wao ndio watakaoweza kuvieleza vyombo vya hujuma au uharibifu utakapotokea ua unaodhamiriwa kufanywa dhidi ya bomba hilo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wakuu wa mikoa nane ambayo bomba hilo litapitia ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Singida, Manyara, Dodoma na Mkoa wa Tanga.

Bomba la hilo la mafuta ambalo litagharibu dola bilioni 3.5, asilimia 80 ya ujenzi wake utafanyika Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi