Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Yazidi Kuimarisha Huduma ya Upasuaji Moyo kwa Watoto
Oct 05, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na:  Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

HUDUMA ya upasuaji wa magonjwa ya moyo kwa watoto katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imezidi kuimarika tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015 hadi sasa.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa JKCI, Naiz Majani alipozungumza na waandishi wa habari.

Dk. Naiz alikuwa akizungumza kuhusu upasuaji ulioanza kufanyika hospitalini hapo siku ya jumatatu kwa watoto waliozaliwa na magonjwa mbalimbali ya moyo.

Alisema JKCI inafanya upasuaji huo ambao unatarajiwa kukamilika kesho  (leo) kwa kushirikiana na madaktari bingwa wenzao kutoka Shirika la Kimarekani la Mending Kids International ambapo jumla ya watoto 28 wamefanyiwa upasuaji kati ya hao 19 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na tisa upasuaji wa kufungua kifua.

 “Huduma za matibabu ya moyo zilianza rasmi kutolewa nchini mnamo mwaka 2008, hadi kufikia 2015 tuliweza kuwafanyia upasuaji watoto 200 pekee utaona hiyo ni ndani ya miaka saba ya kipindi hicho,” alisema.

Aliongeza “Lakini mwaka 2015 tuliona vema kuanzisha kitengo maalumu cha upasuaji kwa ajili ya watoto, hadi kufikia mwaka huu tumeweza kuwafanyia upasuaji watoto zaidi ya 500 hiyo ni ndani ya kipindi cha miaka miwili pekee.

“Kwa hiyo tunaona manufaa makubwa ya kuanzishwa kwa kitengo hiki kwani tumeweza kuokoa maisha ya watoto wengi ambao tungewapoteza, kwa mwaka serikali ilikuwa na uwezo wa kupeleka nje ya nchi watoto 40 hadi 80 kupatiwa matibabu haya,” alisema.

Alisema pamoja na watoto hao, kuna wengine 145 ambao wanasubiri huduma ya upasuaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi