Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taasisi, Makampuni na Mashirika ya Umma 187 yapewa siku 60 kutoa gawio
Nov 24, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika

Taasisi, Makampuni yenye hisa chache za Serikali na Mashirika ya Umma 187 yamepewa siku 60 ili yawaweze kutoa gawio na mchango kwa Serikali, baada ya kushindwa kufanya hivyo leo.

Akizungumza Ikulu jijini Dodoma, katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika Taasisi, Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache na Mashirika ya Umma 79 kati ya 266 ambayo ni shilingi trilioni 1.05, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo leo kuwa anatoa siku 60 kwa  Mashirika 187  ambayo hayajatoa gawio au mchango kwa Serikali ili yaweze kutoa mchango wao.

“Hatuwezi kuendelea kuwa na Mashirika au Taasisi za namna hii, pamoja na wenyeviti wa Bodi, tunazungumza kila mara hawataki kuelewa, licha ya Serikali kuweka fedha kiasi cha shilingi trilioni 59.6 ambazo ni fedha za watanzania kama mtaji katika Mashirika hayo, Waziri Mpango natoa siku 60 kuanzia leo ili Mashirika haya 187 yaweze kukabidhi kwako gawio” Alisema Rais Magufuli.

Alisisiiza kuwa “Waziri Mpango waandikie barua wote ambao hawapo kwenye orodha hii, baada ya siku 60 ambaye hataleta gawio lolote ajihesabu hayupo, kila siku wanasema wanapata hasara, kila siku ni hasara tu, nchi za Scandinavia zinaendesha nchi zao kwa sababu ya gawio, wana watu waaminifu kama nyinyi mlioleta gawio hapa leo”

Rais Magufuli aliwapongeza waliochangia gawio na kusema kuwa waendelee kufanya hivo kwani nchi haiwezi kuwa na maendeleo kwa kujenga miradi kama vile reli ya kisasa, kujenga hospitali na shule au mradi wa Bwawa la Nyerere bila kuwa na fedha ambazo zinakusanywa kupitia vyanzo vya kodi pamoja na gawio au michango.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa anawakumbusha watanzania kuwa uchumi wa Tanzania utajengwa na watanzania wenyewe  na  hakuna mtu atakayekuja kulijenga taifa hili.

Aidha, Waziri Mpango alisema kuwa katika Serikali ya Awamu ya Tano ukusanyaji wa mapato umeongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita.

“Mapato yaliyotokana na gawio na michango ya Kampuni, Taasisi na Mashirika yameongezeka sana ambapo mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi bilioni 161.04 tu, na  mwaka 2017/2018 yalikuwa shilingi bilioni 842.13, na kama hiyo haitoshi mwaka 2018/2019 mapato yamefikia shilingi trilioni 1.05, hili ni ongezeko kubwa sana na linastahili pongezi kwa Serikali yako Mheshimiwa Rais” alisema  Waziri Mpango.

Naye, Msajili wa Hazina, Athumani Mbutuka alisema kuwa Serikali imefanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudhibiti   matumizi katika Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma, ambapo Juni mwaka 2019 Mashirika ya Umma 15 yalipunguzwa hadi kufikia 8 na kupunguza gharama za uendashaji.

Vilevile, aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka huu, Ofisi ya Msajili wa Hazina imevirudisha viwanda 31 vilivyokuwa havifanyi kazi, pamoja na kurudisha Serikali viwanja, mashamba na nyumba 337.

Taasisi, Kampuni na Mashirika 79 yaliyotoa gawio, ambapo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro, Wakala wa Huduma za Misitu na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) yalikabidhiwa cheti kwa kufanya vizuri. Aidha, TPA iliyotoa gawio la shilingi bilioni 169 na TPC iliyotoa shilingi bilioni 14 yalipewa tuzo kwa  kutoa gawio kubwa zaidi.

     

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi