Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jul 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini kufunga na kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (Electronic Fiscal Petrol Printer).

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 19 Julai, 2017 wakati akizungumza na wananchi wa Biharamulo Mkoani Kagera muda mfupi kabla ya kufungua barabara ya lami ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga.

Mhe. Dkt. Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

“Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli pia amewataka wafugaji waliovamia hifadhi ya Burigi Mkoani Kagera kuondoa mifugo yao mara moja na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kuendelea na operesheni ya kuondoa mifugo yote iliyovamia hifadhi hiyo na maeneo mengine yasiyoruhusiwa kupeleka mifugo.

Amewataka wafugaji kote nchi kuchunga mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kulisha mifugo na ameonya kuwa vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo yao katika hifadhi na mashamba ya wakulima havikubaliki.

“Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya simamieni hilo, ninajua bado kuna ng’ombe mle hifadhini, simamieni kwa kuzingatia sheria za hifadhi.

“Kwa hiyo wafugaji wajifunze namna ya kufuga, kama unaona una ng’ombe wengi na huwezi kuwatunza uza, hata mimi nimeuza ng’ombe wangu niliona wamekuwa wengi siwezi kuwatunza, viwanda vipo” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu kero ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Biharamulo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji katika mji huo na amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Maji Taka Bukoba (BUWASA) Alen Mwita kuhakikisha mashine zilizonunuliwa zinafungwa na kuanza kutoa maji ifikapo tarehe 30 Julai, 2017.

Baada ya kuzungumza na wananchi wa Biharamulo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo cha mabasi, Mhe. Rais Magufuli amefungua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga ambayo inaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.

Barabara hiyo ina urefu wa Kilometa 154 na imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 190.4 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli ametembelea Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke alikosoma elimu ya sekondari ambapo ameendesha harambee iliyofanikisha kupatikana mifuko 1,000 ya saruji na mabati 150 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa majengo ya Seminari hiyo, na pia ametoa Shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kutengeneza dirisha la bweni alilolivunja wakati akiwa kidato cha pili pamoja na madirisha mengine yanayohitaji matengenezo.

Akiwa njiani kuelekea Ngara, Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Nyakahura ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itaifanyia matengenezo barabara ya Nyakahura – Rusumo – Ngara, ameahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwenda kuangalia namna ya kutatua tatizo la maji na pia amechangia Shilingi Milioni 10 katika ujenzi wa majengo ya shule.

Kesho tarehe 20 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera ambapo hapa Ngara atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika mchana.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Ngara, Kagera

19 Julai, 2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi