“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea jana usiku katika wilaya ya Igunga mkoani Tabora, nawapa pole wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mkubwa.
“Aidha, nalitaka Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Mamlaka zote zinazohusika na usalama wa barabarani kujitathmini, na kutafuta majawabu ya kwa nini ajali za barabarani zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani?”
Ni sehemu ya salamu za rambirambi na maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Aprili, 2018 kufuatia ajali iliyotokea katika Kijiji cha Makomero, Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora jana tarehe 04 Aprili, 2018 saa 2:00 usiku na kusababisha vifo vya watu 12.
Ajali hiyo imetokea baada ya basi la kampuni ya City Boy lililokuwa limebeba abiria kutoka Karagwe Mkoani Kagera kuelekea Dar es Salaam kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Singida kuelekea Igunga.
Pamoja na kutoa pole kwa wafiwa na kutoa maelekezo hayo, Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi wote wanaohusika na usimamizi wa usalama wa barabarani kutafakari kwa nini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali.
Aidha Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, na amewaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote 46 wapone haraka ili waungane na familia zao katika ujenzi wa Taifa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Aprili, 2018