Waziri Mahiga Afanya Mazungumzo na Mfalme Letsie wa III Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Lesotho
Mkuu wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amemhakikishia Mfalme Letsie wa III wa Lesotho kuwa Asasi ya Ushirikiano ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama imethibitisha pasipo mashaka utayari wa wapiga kura wa nchi hiyo kupiga kura siku ya Jumamosi tarehe 3 Juni 2017.
Hayo yamesemwa kwenye mazungumzo ya viongozi hao ambapo Mhe. Dkt. Mahiga alimuelezea Mtukufu Mfalme Letsie wa III, hatua mbalimbali za uangalizi wa uchaguzi zilizochukuliwa na Jumuiya ya SADC tangu alipofika nchini Lesotho. Jumuiya hiyo mbali na kupeleka waangalizi 41 wa uchaguzi kutoka kwenye nchi tisa wanachama, pia ina wajumbe wawili wa Baraza la Ushauri wa Masuala ya Uchaguzi ambapo mmoja wa wajumbe hao ni Jaji Mstaafu John Tendwa wa Tanzania.
Mhe. Mahiga pia alisifu jitihada za Serikali na Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho ambao kwa pamoja wamehakikisha kuwa mazingira mazuri yameandaliwa yatakayoruhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu kufanyika kama ilivyopangwa.
Kwenye mazungumzo yao, Mhe. Mahiga alitumia pia nafasi hiyo kumpelekea Mfalme Letsie salaam za heshima kutoka kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama ambayo inaundwa na nchi za Tanzania, Msumbiji na Angola kwa sasa.
Kwa upande wake, Mtukufu Mfalme Letsie wa III wa Falme ya Lesotho alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kama kiongozi wa asasi hiyo muhimu ya Jumuiya ya SADC na kuongeza kuwa ni matarajio yake kuwa chini ya uongozi wake makini na mahiri, nchi wanachama wa Jumuiya watatekeleza kwa ufanisi majukumu yao muhimu ya kuendeleza jumuiya.
Mfalme huyo mrithi wa baba yake Mfalme Moshoeshoe wa II anayetawala Lesotho tangu mwaka 1996 kama Falme ya Kikatiba, alisema anaiheshimu sana Tanzania kwa mchango mkubwa kwa nchi hiyo hususan kwenye kuendeleza taaluma mbalimbali nchini humo. Alisema kwa miaka mingi sasa wataalamu wa masuala ya afya na elimu kutoka Tanzania wameendelea kufanya kazi Lesotho na kuongeza kuwa hata yeye binafsi alifundishwa Chuo Kikuu cha Lesotho na Mtanzania masomo ya Sheria na Sayansi ya Siasa.
Mtukufu Mfalme Letsie alimaliza kwa kuahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Lesotho na Tanzania ambapo chimbuko lake ni kuwa nchi zote mbili ni wanachama waanzilishi wa Jumuiya ya SADC. Aidha alionesha nia kubwa ya kuzuru Tanzania siku za usoni, na kumuomba Mhe. Dkt. Mahiga, kufikisha salamu za heshima na ushirikiano kwa Rais na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Maseru, Lesotho 25 Mei, 2017 |