Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Mar 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 13 Machi, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Urusi ulioongozwa na Mjumbe Maalum wa Rais wa Urusi katika masuala ya Afrika ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Mikhail Bogdanov, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Urusi Mhe. Vladimir Putin kwa ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi hiyo na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza inatambua umuhimu wa uhusiano huo na kwamba itauendeleza na kuukuza zaidi hususani katika masuala ya biashara, uwekezaji, utalii na utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na miundombinu.

“Naomba ufikishe ujumbe wangu kwa Mhe. Rais Putin kuwa Watanzania wanaipenda Urusi na tunamkaribisha kuja kutembelea nchi yetu pamoja na wananchi wengine wa Urusi, tunawakaribisha pia wawekezaji waje wawekeza katika fursa mbalimbali zilizopo hapa Tanzania kwa manufaa yetu sote” Mhe. Rais Magufuli amemueleza Mhe. Bogdanov.

Kwa upande wake Mhe. Bogdanov ambaye amewahi kutembelea Tanzania miaka 8 iliyopita ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kasi nzuri ya maendeleoiliyoyapata katika kipindi kifupi na amebainisha kuwa Urusi imedhamiria kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Mhe. Bogdanov amesema Urusi inao mpango mahususi wa kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika kuongeza kasi ya maendeleo na kwamba hivi karibu Tanzania na Urusi zitatiliana saini makubaliano ya kuanzisha tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) katika biashara, uwekezaji na uchumiili rasilimali na fursa zilizopo katika pande zote zitumike kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema mazungumzo hayo yamekwenda vizuri na kwamba Tanzania inatarajia tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Urusi itasaidia kukuza uchumi kupitia madini, gesi na utalii hasa wakati huu ambapo Urusi imeitangaza Tanzania kuwa nchi yenye vivutio bora vya utalii duniani.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi Tanzania nchi Urusi Mhe.Mej Jen. Mstaafu Simon Mumwi na Balozi wa Urusi nchini Tanzania Mhe. Yuri Popov.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu wa Tanzania na Morocco wanaoshughulikia ujenzi wa uwanja wa michezo katika Jiji la Dodoma, unaotarajiwa kujengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI.

Balozi wa Morocco hapa nchini aliyeongoza ujumbe wa wataalamu kutoka Morocco Mhe. Abdelilah Benryane amesema pamoja na kuzungumzia uhusiano mzuri wa Tanzania na Moroccowamejadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa wakati wa ziara ya Mfalme wa Morocco hapa nchini mwaka 2016 ikiwemo ujenzi wa Msikiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa Jijini Dar es Salaam na kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema uwanja huo utajengwa jirani na eneo la Nanenane kando ya barabara ya Dodoma – Morogoro, utajengwa kwa mfano wa mlima Kilimanjaro na utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji kati ya 85,000 na 100,005.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

13 Machi, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi