Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Jun 29, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Dambudzo Mnangagwa wamekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili yenye udugu wa kihistoria ulioasisiwa na Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Mugabe.

Viongozi hao wamefikia makubaliana hayo baada ya kufanya mazungumzo rasmi na baadaye kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam katika siku ya kwanza ya ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Mnangagwa iliyoanza leo tarehe 28 Juni, 2018 hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli amesema mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Zimbabwe ilikuwa na thamani ya Shilingi Bilioni 18.3, mwaka 2017 ilikuwa Shilingi Bilioni 21.1 na kwa ujumla Zimbabwe imewekeza nchini Tanzania kiasi cha Shilingi Bilioni 72.2, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uhusiano wa Mataifa hayo.

Kufuatia hali hiyo Mhe. Rais Magufuli amesema wamekubaliana tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent Commission-JPC) ambayo mara ya mwisho ilikutana mwaka 1998, ikutane mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu ili kujadili vikwazo na kutafuta majawabu ya kukuza biashara na uwekezaji baina ya Mataifa haya mawili.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Mnangagwa kwa kukubali mwaliko wa kuja kutembelea hapa nchini Tanzania ikiwa ni miezi 6 tangu aingie madarakani na akiwa katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu, na amempongeza kwa namna anavyochukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha demokrasia, kukuza uchumi na kumpa heshima Baba wa Taifa la Zimbabwe, Rais Mstaafu Robert Mugabe.

“Nakupongeza kwa namna unavyofanya juhudi za kusukuma mbele maendeleo ya Zimbabwe, na pia nakupongeza kwa jinsi mnavyomthamini Mzee Robert Mugabe na kumpa heshima ya kuwa Baba wa Taifa la Zimbabwe, yeye na viongozi wenzake Julius Nyerere wa Tanzania, Keneth Kaunda wa Zambia, Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Kwame Nkrumah wa Ghana, Patrice Lumumba wa DRC, Samora Machel wa Msumbiji na wengine wametoa mchango mkubwa katika juhudi za ukombozi wa Bara la Afrika, tuna kila sababu ya kuwaenzi na kuwatunza” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mhe. Rais Mnangagwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumualika na amesisitiza kuwa Zimbabwe inatambua mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Taifa hilo pamoja na mataifa mengine ya Afrika ambayo yaliendesha harakati zao za ukombozi nchini Tanzania.

“Nakumbuka miaka 50 iliyopita nilipokuja hapa Tanzania pamoja na wenzangu akiwemo Rais Mstaafu Mugabe, tuliweka kambi yetu ya chama cha FRELIMO kule Bagamoyo na pia wenzetu wengine walikuwa Iringa na Mbeya, kwa hiyo kwetu sisi Tanzania ni Mama yetu, kamwe hatutaisahau na tutahakikisha vizazi vyetu vinatambua mchango huu mkubwa wa Tanzania” amesema Mhe. Rais Mnangagwa.

Mhe. Rais Mnangagwa ameahidi kuwa Zimbabwe ipo tayari kukuza ushirikiano wake na Tanzania katika kuimarisha biashara na uwekezaji hususani katika kilimo, utalii, usafiri wa anga, madini pamoja na ulinzi na usalama, na kwamba tangu aingie madarakani wafanyabiashara wa Tanzania wamejitokeza kuwekeza nchini Zimbabwe na kumekuwa na ongezeko kubwa la uwekezaji wa mitaji nchini humo kutoka nchi za nje.

“Baada ya kufanya maboresho ya sera zetu hususani sera ya ardhi ambapo tulilazimika kuchukua ardhi ambayo kwa sehemu kubwa ilikuwa ikimilikiwa na wageni kwa lengo la kuleta usawa wa umiliki na wazawa ambao hawakuwa na ardhi, tuliwekewa vikwazo vingi na Mataifa ya nje, tunashukuru nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walituunga mkono, katika kipindi hicho uchumi na sarafu yetu ilianguka, lakini sasa tangu niingie madarakani tumefungua milango ya uchumi, vikwazo vinaondolewa na uchumi unakuwa kwa wastani wa asilimia 4.2 kutoka 0, na mwaka huu tunatarajia utaongezeka kufikia asilimia 5” amesisitiza Mhe. Rais Mnangagwa.

Baadaye leo Mhe. Rais Mnangagwa atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

28 Juni, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi