Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
May 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais Magufuli Azungumza na Wanafunzi wa SUA,  Atoa Pongezi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kufanya utafiti na kutoa mafunzo bora ya kilimo yaliyojenga heshima kwa Taifa na kuleta mageuzi katika kilimo, ufugaji na uvuvi.

Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo terehe 07 Mei, 2018 alipokitembea Chuo Kikuu cha SUA na kuzungumza na jumuiya ya wanafunzi na wafanyakazi ambapo amewahakikishia kuwa kwa kutambua dhamira ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipoanzisha chuo hicho, Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha inaimarisha miundombinu, vitendea kazi na kuwezesha utafiti zaidi utakaochangia katika juhudi za kuimarisha uchumi hasa viwanda.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda kuendelea kufanya mabadiliko ya kukiimarisha, na ameahidi kutoa matrekta 10 yatakayotumika katika mafunzo.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekipongeza Chuo Kikuu cha SUA kwa utafiti wake wa kipekee duniani wa kumtumia mnyama panya kugundua ugonjwa wa kifua kikuu na kugundua mabomu, na pia amekipongeza kwa kuanzisha mashamba ya mazao ya mfano yenye ukubwa ekari 300 na shamba la mipapai ambayo inazaa matunda baada ya muda mfupi wa miezi 5 tangu kupandwa.

Mhe. Rais Magufuli amezungumzia madai kuwa ubora wa elimu nchini umeshuka na kusisitiza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha SUA, kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kutoa elimu bure iliyoongeza udahili wa wanafunzi na upelekaji wa fedha za maendeleo katika vyuo na shule mbalimbali vinainua kiwango cha elimu ikilinganishwa na nchi ilikotoka.

Mhe. Rais Magufuli amepokea na kujibu kero mbalimbali zilizotolewa na wanafunzi na wafanyakazi wa SUA ambapo ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhamisha Shilingi Bilioni 2 zilizopangwa kupelekwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya miradi ya maendeleo na badala yake fedha hizo zipelekwe SUA kwa ajili ya kujenga mabweni ya wanafunzi ambao wanataabika kusafiri umbali mrefu kutafuta makazi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo kote nchini kujikita katika masomo wawapo vyuoni, badala ya kujihusisha na masuala ambayo ni kinyume na masomo kama vile kugeuza vyuo kuwa uwanja wa siasa na ameonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kuwafukuza vyuoni wanafunzi watakaojihusisha na vitendo vya vurugu.

Mapema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa Serikali kuanza kupeleka fedha za maendeleo katika vyuo vikuu kwa ajili ya kujenga miundombinu muhimu, ambapo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 SUA imepata shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa maabara, na amebainisha katika mwaka huu chuo hicho kimetengewa Shilingi Bilioni 8 kwa ajili ya kujenga madarasa ya mihadhara, jengo la shule kuu ya biashara, ofisi ya walimu, madarasa na ukumbi wa matumizi mtambuka, ikiwa ndio chuo kilichopata fedha nyingine kuliko chuo kingine chochote hapa nchini.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda amesema chuo hicho chenye wanafunzi 9,384 kimedhamiria kuendelea kufanya utafiti utakaosaidia kuinua tija katika kilimo, ufugaji, uvuvi na misiti ili kufanikisha sera ya viwanda, na kwamba kwa kuanzia wasomi wa SUA wanashiriki ipasavyo katika uzalishaji wa miwa katika mashamba ya kiwanda kikubwa cha sukari cha Mkulazi Mkoani Morogoro.

Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli amemaliza ziara yake Mkoani Morogoro na kurejea Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Morogoro

07 Mei, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi