Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
May 03, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais Magufuli afungua barabara ya Iyovi - Iringa - Mafinga, na afungua kiwanda cha Silverlands

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Mei, 2018 amefungua barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6 ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Dar es Salaam – Tunduma (TANZAM), inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za kusini mwa Afrika zikiwemo Zambia, Zimbabwe, Kongo-DRC na Malawi.

Sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo zimefanyika katika eneo la Ihemi, Iringa Vijijini na kuhudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Naibu Balozi wa Denmark hapa nchini Bi. Camilla Christensen, Wabunge, viongozi wa dini na viongozi wa siasa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara hiyo umegharimu Shilingi Bilioni 282 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Serikali ya Denmark kupitia Shirika lake la misaada (DANIDA) na Shilingi Bilioni 1.8 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amesema mbali na barabara hiyo Denmark imeshirikiana na Tanzania kukarabati barabara za Ubungo - Mlandizi(kilometa 60.7), Chalinze – Melela (kilometa 129) na Chalinze – Segera – Tanga (kilometa 246.7) na amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hizo kutasaidia kuimarisha usafiri na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na biashara.

Naibu Balozi wa Denmark hapa nchini Bi. Camilla Christensen ameelezea kufurahishwa kwake na kukamilika kwa ujenzi huo na amesisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na Denmark ulioanza miaka 50 iliyopita utaendelea kudumishwa hususani katika vipaumbele vinavyohusu uchumi na fedha, afya, ajira na uboreshaji wa biashara.

Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Denmark kwa kufadhili miradi mbalimbali ukiwemo ujenzi wa barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga ambayo itasaidia kuboresha maisha ya watu kwa kuwarahisishia kupata masoko ya mazao na bidhaa zao pamoja na kukuza uzalishaji mali.

“Ndugu zangu wananchi wa Iringa, barabara hii imekamilika na ni miongoni mwa barabara bora tulizonazo hapa nchini kwetu, natoa wito kwenu mchangamkie fursa, limeni mazao ya kutosha na myasafirishe kwenda kwenye masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameiomba Denmark kupitia DANIDA kufadhili ujenzi wa barabara ya Igumbiro – Kihesa yenye urefu wa kilometa 11 ambayo itasaidia magari yatokayo kusini mwa Tanzania kwenda Dodoma kutopita katikati ya Mji wa Iringa ili kuepusha msongamano na athari za ajali za magari zinazoweza kutokea.

Mapema asubuhi Mhe. Rais Magufuli amefungua kiwanda cha kutotoresha vifaranga na kuzalisha chakula cha kuku cha Silverlands kilichopo Ihemi, Iringa Vijijini.

Mkurugenzi wa Silverlands Dkt. Ben Moshi amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vifaranga 150,000 kwa wiki na tani 40 za chakula cha kuku kwa saa, na kwamba mwaka huu kimezalisha vifaranga 7,200,000 ambavyo vimeuzwa ndani ya nchi na nchi nyingine zikiwemo Ethiopia, Kenya, Nigeria na Uganda.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema uwepo wa kiwanda hicho utawasaidia wakulima kupata soko la mazao kwani kinahitaji tani 120,000 za mahindi kwa mwaka na tani 40,000 za soya, na amesisitiza kuwa teknolojia inayotumika inamwezesha mfugaji kuzalisha kuku bora wasiokuzwa kwa kutumia dawa na virutubisho vya kikemikali.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wawekezaji wa kiwanda cha Silverlands kwa uwekezaji mkubwa wa Dola za Marekani Milioni 71 na kutoa ajira kwa watu 938 lakini amewataka kulipa kodi za Serikali kama inavyopaswa badala ya kusingizia kuwa hawapati faida.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Iringa

03 Mei, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi