Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa Fupi ya Ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa
Feb 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewasili nchini Ufaransa kwa ziara ya kikazi iliyoanza tarehe 10 Februari 2022 kwa mwaliko wa Mhe. Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Bahari Kuu (One Ocean Summit) uliofanyika tarehe 11 Februari 2022, Brest, Ufaransa.


Pembezoni mwa Mkutano huo, Mhe. Rais amefanya mazungumzo na Bw. Henri-Max Ndong Nzue, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Total Energies Kanda ya Afrika ambapo walijadili kuhusu Utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) linalojengwa kutoka maeneo ya Kabaale–Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania.

Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Gharama za kukamilisha ujenzi wa mradi wa bomba hilo zinatarajia kufikia takribani Shilingi Trilioni 8 za Kitanzania.

Mhe. Rais amemhakikishia Bw. Ndong Nzue kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kwa utekelezaji wa Mradi huo na kwamba tayari imetekeleza vipengele muhimu katika mkataba wa mradi huo.


Mhe. Rais pia alishuhudia uwekaji saini Mikataba (Agreements), Hati (Memorandum of Understanding - MoU) na Matamko (Declaration of Intent) kuhusu ushirikiano kwenye ufadhili wa miradi ya maendeleo na utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini Tanzania.

Katika Mikataba hiyo, Serikali itanufaika na mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Euro Milioni 178 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mabasi ya mwendokasi na Euro Milioni 80 ili kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Aidha, Tanzania na Ufaransa zimesaini matamko ya dhamira ya kushirikiana kwenye maeneo ya uchumi wa buluu na usalama baharini.

Sambamba na hilo, Mhe. Rais pia ametembelea Kampuni ya Ocea ambayo inajishughulisha na utengenezaji wa meli na Kituo cha Sayansi na Kilimo (Station F Start Up Facility) kinachojishughulisha na kutoa fursa kwa wajasiriamali wadogo kupata elimu na ubunifu wa kibiashara, fursa za mitaji masharti nafuu na masoko.

Mhe. Rais pia atakutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Ufaransa leo na kunzungumza nao kuhusu masuala mbalimbali ya Maendeleo nyumbani.

Ratiba ya Mhe. Rais hapa Paris itaendelea kesho ambapo anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Mhe. Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa; Mhe. Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UNESCO; na kuhutubia Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ufaransa MEDEF.

Ziara ya Mhe. Rais nchini Ufaransa itahitimishwa tarehe 14 Februari 2022 mchana, ambapo ataendelea na ziara nchini Ubelgiji.

Akiwa Brussels, Ubelgiji Mhe. Rais atafanya mazungumzo na Mhe. Charles Michel, Rais wa EU Council, Dr. Georges Rebelo Chikoti, Katibu Mkuu wa OACPS, kuhutubia Mabalozi wa wa Umoja wa OACPS wanaowakilisha nchi zao Ubaligiji na baadaee atashiriki kwenye Mkutano wa Sita (6) wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika (6th EU - AU Summit) unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 na 18 Februari 2022.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi