Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAA Yawapiga Msasa Wanausalama Wake
May 14, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_31656" align="aligncenter" width="1000"] Washiriki, Wakufunzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Joseph Nyahende (wa pili kushoto waliokaa) wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo inayosafiri kwa ndege za mizigo iliyoanza leo kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo kwenye jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).[/caption]

Na Bahati Mollel - TAA

Wanausalama 18 kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wametakiwa kuzingatia mafunzo ya Usalama wa vifurushi na mizigo vinavyosafirishwa kwa ndege za mizigo yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo kwenye jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Joseph Nyahende, ambapo ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia zaidi kuongeza uelewa wa vifurushi na mizigo hiyo inayosafirishwa bila kuambatana na abiria.

“Tuna nia njema ya kuwatengeneza wanausalama wetu na hili darasa ni muhimu sana kwa ajili yenu, hivyo tunahitaji mjifunze kwa faida yenu binafsi, taasisi na taifa kwa ujumla kwani hamtaweza kuruhusu vitu visivyostahili kupita kwani mtakuwa sasa mmepata mafunzo ya kuvitambua,” alisema Bw. Nyahende.

Naye mmoja wa wakufunzi Bw. Sunday Mweemba kutoka Zambia ameishukuru menejimenti ya TAA ya kuomba kozi hiyo kupitia taasisi ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), ambayo itawafanya wanausalama wake kutambua vitu vingi vinavyofanyika katika viwanja vingine Duniani.

“Tumeona ni jinsi gani menejimenti yenu ilivyojitoa kwa ajili yenu, na hii inatolewa na ICAO na kupitia kazi yenu mnatakiwa kuwa makini zaidi na kuzijua sheria zote zinazohusika na mizigo, na tuna matumaini hadi mwisho mtakuwa mmeweza kujijengea uwezo,” alisema Bw. Mweemba.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Usalama wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Julius Misollow alisema mafunzo hayo ni ya kwanza, ambapo yana lengo la kuwajengea uwezo wanausalama katika kukagua vifurushi na mizigo inayosafirishwa yenyewe bila abiria kwa kutumia ndege za mizigo.

“Magaidi wamekuwa wakitumia njia mbalimbali na wengine wanatumia mizigo au vifurushi kufanya hujuma, hivyo tunaimani kwa mafunzo haya tutawajengea uwezo wa kutambua mizigo ambayo ni hatarishi, ingawa kwa Tanzania haijawahi kutokea tatizo hilo,” alisema Bw. Misollow.

Hata hivyo, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mitihani na watakaofaulu kwa alama 70 wataendelea na kozi ya ukufunzi ambayo itaanza baadaye kuanzia Mei 19, 2018.

Washiriki wanaoshiriki na viwanja wanavyotoka ni pamoja na Philbert Lyimo, Ahmed Zomboko, Thawabu Njeni, Rehema Mlanzi, Nuhu Kisweswe, Martha Kilunga, Levina Valasa, Josephine Kahimba, Anna Myovela, Fatma Shomari na Stephen Ntambi (JNIA); Zalia Msangi na Stephen Magambo (Arusha).

Wengine ni Mathias Gombo, Lilian Malero na Wenceslaus Sango (Mwanza); Bebedict Ole Laput (Songwe); na Felister Lutonja (Shinyanga).

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi