Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema vijana wote nchini wana deni la kuhakikisha wanausimamia, wanaulinda, wanauimarisha na kuutetea muungano kwa manufaa ya Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo.
Akizungumza kwenye dua na maombi ya miaka 60 ya muungano leo jinini Dodoma, Mhe. Abdulla amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kudumisha amani.
"Zipo nchi ambazo zilijaribu kuungana lakini hata miaka 20 hawakufika. Sisi tuna imani kuwa tutaendeleza muungano kwa kusimama imara kuulinda, kuujenga na kuutetea pamoja na kufanya mambo yote kuhakikisha muungano unaendelea kudumu," amesimulia Mhe. Abdulla.
Naye, Waziri wa Nchi - Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema kutimiza miaka 60 ya muungano sio jambo dogo hivyo Watanzania wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu.
"Mwaka 2006, Rais wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Mrisho Kikwete alianza mchakato wa kujadili hoja za muungano, zilikuwa 25 wakati huo, mwaka 2010 zilitatuliwa hoja mbili tu, mwaka 2020 zilitatuliwa hoja tano ikiwa ni jumla ya hoja saba na kubaki hoja 18," amehadithia Dkt. Jafo.
Waziri Jafo amesimulia kuhusu kero zilizosalia akisema: "Chini ya uongozi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zimetatuliwa zaidi ya hoja 15, hivyo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutupa viongozi wote hawa wanaoshughulikia masuala ya muungano."
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unatimiza miaka 60 tangu ulipoasisiwa rasmi Aprili 26, 1964 huku ukiwa muungano pekee uliodumu kwa miaka mingi barani Afrika.