Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

SMZ Kutumia Mabadiliko ya Kidigitali Kuinua Uchumi wa Buluu-Rais Mwinyi
Oct 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Tuzo Maalum kwa pamoja na Mawaziri wa SMZ na SMT (kulia kwa Rais) ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania, Mhe. Nape Nnauye na (kushoto kwa Rais) ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Mhe.Dkt. Khalid Salum Mohamed, baada ya ufunguzi na kukabidhi Kituo cha TEHAMA Bwefum Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo tarehe 26-10-2022.

Na Grace Semfuko, MAELEZO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali yake imedhamiria kutumia mabadiliko ya kidigitali katika kuinua na kukuza uchumi wa bluu lengo likiwa ni kuongeza pato kwa Wananchi na Pato la Taifa kupitia mazao bahari.

Ameyasema hayo leo Oktoba 26,2022 wakati akifungua Kongamano la sita la Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa nchini Tanzania linaloendelea kwa siku tatu Mjini Unguja.

"Katika Muongo uliopita, nchi mbalimbali Duniani zimeonesha ongezeko kubwa la matumizi ya rasilimali Bahari na Maziwa katika kuimarisha uchumi wa buluu, hii imetokana na kuwa nchi zimeanza kutambua kuwa bahari na maziwa yetu ni hazina na utajiri mkubwa kwa upande wa rasilimali mbalimbali", amesema Rais Mwinyi.

Amesema kwa upande wa Zanzibar Serikali imeanza kutambua nafasi ya uchumi wa buluu katika kukuza maendeleo na kwamba inazingatia usimamizi bora wa Mazingira na rasilimali za bahari.

"Kwa upande wa Afrika, rasilimali zetu za bahari na majini ni muhimu katika kufikia ajenda 2063, hivyo basi, kaulimbiu ya mkutano huu inayosema 'Kutumia Mabadiliko ya Kidigitali katika Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi' inaendana na mipango ya kinaendeleo ya nchini kwetu, Serikali ninayoiongoza inatambua nafasi ya uchumi wa buluu katika kukuza maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi kupitia usimamizi bora wa rasilimali za bahari ", amesema Rais Mwinyi.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema maendeleo ya TEHAMA yameifanya Sekta ya Mawasiliano nchini kukua kwa kiwango kikubwa kiuchumi huku Tanzania ikiendelea kuchaguliwa kuingia katika mabaraza na kamati mbalimbali za Kimataifa kutokana na kuwepo kwa mabadiliko makubwa na mazuri ya sekta hiyo.

"Maendeleo ya Sekta ya TEHAMA yameifanya Sekta ya Mawasiliano Nchini kukua kwa asilimia 9.1% mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 8.4% ya mwaka 2020, ukuaji huu ni wa wastani wa asilimia 8% kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2016 mpaka mwaka 2021, hii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi na kuchangia Pato la Taifa", amesema Mhe. Nape.

Amesema kadi za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka kadi milioni 40 kwa mwaka 2016 hadi kufikia milioni 58 mwezi Septemba mwaka huu wa 2022 ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 8% kila mwaka na kubainisha kuwepo pia kwa ongezeko la watumiaji wa internet kutoka milioni 19.8 kwa mwaka 2016 hadi kufikia milioni 31 kwa mwezi Septemba mwaka huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi