Na Mwandishi Wetu
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa mafunzo kwa watumishi wote wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, juu ya alama zinazopatikana katika noti halali za fedha za Tanzania.
Akitoa mafunzo hayo leo kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Afisa Kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Rehema Zongo amewafafanulia watumishi hao namna ya kutambua noti halali kwa vitendo huku akisisitiza alama muhimu zinazopatikana katika noti halali ili waweze kutofautisha na zile bandia.
Zongo alisema watumishi wanatakiwa kuichunguza noti halali kwa kuipapasa ili kuhisi mparuzo kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalumu yanayoonesha thamani halisi ya fedha.
Amewasisitizia kuwa wanaweza kuitambua noti halali kwa kuangalia sura ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayoonekana unapoimulika noti kwenye mwanga na pia kukagua utepe maalumu kwenye noti za shilingi 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 unaoonekana kama madirisha yenye umbo la almasi ambapo hubadilika badilika noti inapogeuzwa geuzwa.
“Ukipata noti bandia au hata kama unaishuku kuwa ni bandia, ipeleke benki au kituo chochote cha polisi kilichopo karibu nawe. Lakini pia tuwe na utaratibu wa kuthibitisha uhalali wa noti mara tuzipatapo kwa kuzingatia alama tulizo wafundisha”, alisisitiza huku akiwaomba kutoa elimu ya utambuzi wa noti halali kwa wananchi wengine.
Zongo amewafahamisha watumishi hao kuwa kitendo cha kughushi pamoja na kumiliki fedha bandia kwa nia ya kuzitumia ni kosa la jinai linalosababisha mhusika kushitakiwa kwenye vyombo vya sheria.
Akiongea kwa niaba ya wafanyakazi waliopata mafunzo hayo, Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, George Kulwa ameishukuru Benki hiyo kwa kutoa mafunzo na kusema kuwa elimu waliyoipata itawasaidia pia wananchi kwa ujumla kwakuwa watumishi hao watakuwa mabalozi wa elimu hiyo.
Aidha ameiomba benki kuu kuendelea kutoa elimu hiyo mpaka ngazi za vijiji ili taifa lote liwe na elimu sahihi na ya kutosha juu ya alama za noti halali.