Na Dkt Hassan Abbasi*
Mei 3, 2017 wanahabari hapa nchini wanaungana na wanahabari wenzao kote Duniani kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani. Nikiwa mwanataaluma hii, kwanza nawapongeza wanatasnia wenzangu kwa kuadhimisha siku hii mujarabu.
Pili, ni matarajio yangu kuwa wanahabari hasa wa nchini, pamoja na kupiga kelele kuhusu maslahi na haki zao kama ilivyo kawaida, safari hii wataitumia siku hii kujitazama upya namna wanavyotekeleza wajibu wao kwa jamii.
Hata kauli mbiu ya waasisi wa siku hii inadhihirisha hoja na haja hii ya kujitazama upya. Kaulimbiu ya mwaka huu iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inasomeka: “Critical Minds for Critical Times: Media’s role in advancing peaceful, just and inclusive societies.”
Kauli mbiu hii, kwa mtazamo wangu, na hata uchambuzi wa wanahabari wengi nguli duniani, kwa kifupi inalenga sana kusisitizia umuhimu wa kuwa na wanahabari wenye akili (critical minds).
Lakini si wenye akili tu kwa kuwa na uwezo wa kuchambua habari na kufuata misingi ya taaluma yao, sehemu ya pili ya kauli mbiu inachagiza hoja ya wajibu wa wanahabari kwa jamii hasa katika mawanda ya amani na maendeleo ya jamii (Media’s role in advancing peaceful, just and inclusive societies).”
Nawapongeza UNESCO kwa kuja na mada hii aushi kabisa inayosadifu kile ambacho wengi tumekuwa tukijiuliza: Je, licha ya kulalamikia uhuru na haki zao, vyombo vya habari vya leo vinatimiza wajibu wao kwa umma?
Je, vimekuwa sehemu ya kuchagiza maendeleo au kuendekeza siasa za kuzuia maendeleo ya watu? vinafanya nini kuchangia jamii yenye maendeleo endelevu?
Ni mtazamo wangu, na wa wanahabari wengi nguli duniani na hata wananchi wa kawaida kuwa tukijaribu kutafuta majawabu ya maswali haya tutapata majibu yenye kupishana sana. Yapo maeneo lazima tuwapongeze wanahabari, wameitumia na kuitumikia vyema tasnia lakini pia yapo maeneo tumetetereka sana.
Ndio maana, akiichambua kaulimbiu ya mwaka huu, mwandishi nguli wa gazeti la New York Times, Jim Rutenberg, anabainisha kuwa moja ya changamoto inayowahitaji wanahabari kujitafakari mwaka huu ni kuibuka kwa habari zisizofuata maadili wala kujali ukweli, akirejea dhana mpya katika taaluma ijulikanayo kama “fake news.”
Anasema ni wakati sasa wanahabari kujitathmini na kurejea katika uandishi wa kweli na mahiri wa habari akisisitizia: “Na wakifanya hivyo, watakuwa wamefanya uandishi wa habari wa kweli na utakaoiokoa taaluma ya habari (good journalism that saves journalism.”
Niseme tu nikiwa nimepata fursa ya kuwa mwanahabari kwa muongo mmoja hivi na sasa nikielekea katika muongo mwingine wa kuwa katika upande wa pili wa habari-mtoa habari na msimamizi wa sekta ya habari, nimeshuhudia mengi yanayojuzu wanahabari tujikosoe na kujisahihisha.
Kwa kuwa leo tunajikosoa ili kujisahihisha yale mazuri mengi tunayoyafanya tuyaweke pembeni. Tuangalie wapi tunapaswa kuboresha. Tujikite katika changamoto zetu na tunatokaje hadi kurejea kuwa “critical minds.”
Katika makala haya na siku hii ningeweza kuainisha jinsi uandishi wetu unavyokiuka misingi ya uandishi wa habari, jinsi leo tulivyo na waandishi wasiohoji wala wasioenzi misingi adhimu ya taaluma. Lakini nimeona kubwa zaidi, walau kwa uzoefu wangu mpaka sasa, ni moja.
Nalo ni ugonjwa unaoenea kwa wanahabari wengi kutoelewa vyema au kuamua kufumbia macho misingi ya nadharia kuu za kifikra zinazoongoza taaluma yenyewe, nadharia mbili ambazo ni ile ya uhuru wa kujieleza (freedom of expression) na uhuru wa wanahabari (press freedom theory).
Tatizo kubwa na matatizo mengi ya kimaadili katika sekta ya habari na dhana ya “fake news” vinaanzia hapo. Kumeibuka aina ya waandishi wanaoamini kuwa wanaweza kuandika chochote, wakati wowote na juu ya yeyote na kwa namna yoyote ile bila kujali haki na staha za wengine.
Ni kwa sababu ya mitazamo kama hii basi unakutana na waandishi kama Nyamnjoh (2005) katika tasnifu yake “Africa’s Media, Democracy and the Politics of Belonging,” wakilalamikia kushamiri kwa uandishi wa kuchochea ukabila, udini, itikadi za kisiasa au kutetea waovu kwa sababu za kinasaba.
Ni kwa sababu pia ya uandishi wa habari kuonekana ni fani ya mtu anayeitamani tu basi kuingia na kuanza kuandika chochote na atakavyo ndio maana waandishi kama Lawrence Kilimwiko katika andishi lake “Media Power and Politics in Tanzania: Critical Analysis of Media Trends and Practice” analalamikia uandishi wa kuzusha tu habari na kupaka matope watu.
Huu ulevi unaochangiwa pia na wanaharakati na waandishi wenyewe wasioelewa kwa kina haki na wajibu wa kazi na taaluma yao na kuona kwamba uhuru wao haupaswi kuhojiwa wala kudhibitiwa (vinginevyo ni kuingilia uhuru wa habari).
Dhana hii haina mantiki na naomba leo, tukiwa tunatafakari “critical minds” katika taaluma hii, tukumbushane ukweli kwamba iwe ni fani au taaluma kamili, uandishi wa habari haujawahi kuwa jambo huru la mtu kuandika anachotaka bila kujali misingi iliyowekwa.
Kutoka wanafalsafa wa kale kama Plato, wanamageuzi na watetezi wa uhuru wa kujieleza kama John Stuart Mill hadi wanasiasa watetezi wa uhuru wa habari kama Thomas Jefferson na Mahatma Gandhi, wote hawa wanasema uandishi wa habari wa “fake news” haufai. Tusikilize nasaha zao.
Wanafalsafa na Uhuru wa Kujieleza
Inafahamika kuwa wanafalsafa wa kale ni miongoni mwa waasisi wa haki mbalimbali za kiraia, kisiasa na kijamii na kwamba wanakubalika kuwa waasisi pia wa uhuru wa kujieleza.
Katika kujenga hoja yangu kwamba uhuru wa habari una ukomo, nitawatumia wanafasalafa wawili; mmoja wa zama za kale zaidi (ancient philosopher) na mmoja wa zama za hivi karibuni za kimageuzi (enlightenment philosopher).
Tuanze na mwanafalsafa wa kale, Plato, ambaye anajulikana sana katika ulimwengu wa kujenga hoja. Ingawa baadhi ya wasomi wanasema Plato hakuchukua sana muda wake kuainisha masuala ya uhuru wa mawazo lakini yapo matukio au maeneo ambapo Plato aligusia hili.
Katika kitabu chake maarufu kiitwacho “Republica,” ambapo amesisitiza hoja na haja ya kusema ukweli lakini pia kutoeneza uongo na chuki kwa kiwango cha kuiharibu jamii, Plato anaandika bayana kuwa wanaoeneza uongo (of liar poets and storytellers) lazima wazuiwe kufanya hivyo.
Kutoka zama za kale tunaweza pia kujifunza kitu katika zama za mageuzi ya kifikra katika karne ya 19 (enlightenment period). Hapa tunakutana na mwanafalsafa anayekubalika duniani kuwa “Baba wa Uhuru wa Habari/Kujieleza” Mwingereza John Stuart Mill.
Mill (1806-1873) atakumbukwa kwa kueleza nadharia mbalimbali za kusisitizia uhuru wa mawazo na wa vyombo vya habari kuwa lazima uwepo ili kusaidia katika kukuza demokrasia na moja ya nukuu yake mashuhuri ya kutetea haki hizi inasema:
“If all mankind minus one were of one opinion, and only one person was of the contrary opinion, mankind would be no more justified in silencing that one person, than he, if he had the power, would be justified in silencing mankind.”
Akimaanisha kuwa hata kama wanadamu wote wangekuwa na mtazamo kuhusu jambo fulani lakini mmoja wao akawa na mawazo tofauti, dunia nzima haipaswi kumnyamazisha huyo mmoja, na kama ingewezekana, basi ni huyo mtu mmoja ndiye angepaswa kuinyamazisha dunia!
Lakini pamoja na kupigania kwake huko haki na uhuru wa habari na mawazo, Mill kwa upande wake amepata kukiri kuwa uhuru huo una mipaka na kwamba mtu hawezi tu kukurupuka na kuongea/kuandika hata yanayowadhuru wengine.
Akiandika katika fasihi yake mashuhuri duniani “On Liberty” anasema: “The only freedom which deserves the name is that of pursuing our own good in our own way, so long as we do not attempt to deprive others of theirs, or impede their efforts to obtain it.”
Kwamba uhuru kamili wa kujieleza utakuwa hivyo iwapo tu haudhuru haki za watu wengine na wala hautawazuia watu wengine kufurahia haki zao. Huu ni msisitizo kuwa uhuru wa habari una ukomo.
Wanafalsafa wa Kisiasa
Nimeona pia katika muktadha huu tuangalie jinsi wanasiasa mashuhuri duniani ambao pia wanakubalika kuwa sawa na wanafalsafa nao walivyoainisha kuhusu uhuru wa habari na mipaka yake.
Nianze na mmoja wa waasisi wa Taifa la Marekani, Thomas Jefferson.Kwa wasiomfahamu kiongozi huyu, basi mintaarafu tu, ndiye kiongozi wa kisiasa, kwa mapenzi yake katika uhuru wa watu na wa habari, alipata kunukiliwa akisema angetamani vyombo vya habari viwepo lakini serikali isiwepo.
Jefferson aliyaeleza mapenzi yake hayo makubwa namna hiyo juu ya uhuru wa kujieleza na habari katika barua yake ya Januari 16, 1789 kwenda kwa rafiki yake kipenzi Kanali Edward Carrington, akiandika:
"The basis of our government being the opinion of the people, the very first object should be to keep that right; and where it left to me to decide whether we should have government without newspapers, or newspapers without a government, I should not hesitate a moment to prefer the latter."
Hata hivyo, naye pamoja na mapenzi yake hayo yasiyomithilika, kama wanafalsafa wengine, aliamini kuwa uhuru huo una mipaka.
Katika barua yake kwenda kwa rafiki yake mwingine mkubwa, James Madison, wakati wa mjadala nchini Marekani kuhusu haki za kiraia, Jefferson alitaja mambo yanayoweza kuwa kizuizi cha uhuru wa habari kuwa ni pamoja na:
“Matendo yanayoweza kusababisha madhara kwa uhai wa mtu, uhuru wao kwa ujumla, mali zao au kushambulia heshima ya mtu au kuharibu amani na utulivu na ushirikiano wetu wa mataifa.”
Mbali ya Jefferson, Mahatma Gandhi anafahamika kuwa mpigania uhuru wa aina yake na Baba wa Taifa la India. Anakumbukwa kwa namna alivyotoka kuwa mwanahabari hodari, mwanasheria hodari na kisha kuwa mpigania uhuru hodari akitumia falsafa yake ya kutotumia nguvu.
Pamoja na ukweli huo Gandhi aliamini kuwa uhuru wa kweli wa kujieleza na kwamba taaluma ya habari ikiwa fani adhimu lazima watu wake wajue kuwa kalamu isiyotumika kwa umakini haijengi bali hubomoa. Aliandika:
“Freedom of the press is a precious privilege that no country can forego….The sole aim of journalism should be service…even so an uncontrolled pen serves but to destroy.”
Ningeweza kuendelea kuwataja wanamageuzi ya kisiasa na wengineo walioweka misingi mizuri kuhusu wajibu wa wanahabari lakini yatosha tu kwa leo kuhitimisha kwa kutaja mtazamo wa kimataifa kuhusu dhana hii.
Jumuiya ya kimataifa nayo katika kupambana na “fake news” hasa baada ya matukio ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliweka misingi ya kisheria katika kupambana na tatizo hili.
Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia (1966) inashadidisha uhuru wa habari lakini pia inataja masuala makubwa manne ambayo ni ukomo wa haki ya kujieleza/habari.
Masuala yanayohusu kukiuka misingi ya amani, usalama wa nchi, afya ya umma, haki ya faragha na haki ya mtu kutovunjiwa heshima yake yameainishwa.
Ndio maana katika mataifa yote, hata tunayoyaona kuwa yamestaarabika zaidi, watu wamepata kufikishwa mahakamani kwa kukiuka haki hizi na wapo wanaosakwa mpaka sasa na mifano ya akina Julian Paul Assange wa WikiLeaks na Edward Joseph Snowden inatosha katika hili.
Ni kwa hoja hizi basi nihitimishe kwamba taaluma ya habari ni adhimu na adimu sana lakini tuitendee haki kwa kutimiza wajibu wetu huku tukienzi misingi ya ukomo unaolenga kulinda haki za wengine.
Kwa Tanzania tutimize wajibu wetu kama “critical minds” na pia tutimize wajibu wetu katika kuifanya kalamu yetu kuchangia katika maendeleo ya Taifa hususani wakati huu Serikali yetu ya Tanzania ambapo imetunga sheria muhimu sana; Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016 inayosisitizia kwa kina haya niliyoyaeleza.
Nawatakia maadhimisho mema na tafakuri njema.
*Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO. Anapatikana kwa baruapepe: mih@habari.go.tz.