Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Shilingi Bilioni 1.5 Zatengwa kwa ajili ya Mfuko wa Sanaa na Utamaduni
Mar 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Shamimu Nyaki- WUSM, Dodoma

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa takriban kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo na ruzuku kwa wadau wa utamaduni na Sanaa.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Machi 16, 2022 Mtumba jijini Dodoma katika mkutano wa Waandishi wa Habari wakati akieleza Mafanikio ya Mwaka Mmoja ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambapo lengo ni kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo na mitaji katika kuboresha kazi zao huku akieleza kuwa tayari Bodi ya kusimamia mfuko huo pamoja na sektratieti imeanza kufanya kazi.

“Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mhe. Rais  Samia na Watanzania wote kwa ujumla kwa mafanikio ambayo katika mwaka mmoja huu tumeyapata ikiwa ni matokeo ya utashi wa kisiasa wa viongozi wetu na ushirikiano wa Wataalamu mbalimbali wa Wizara yetu na sekta nyingine. Hatimaye leo ndani ya mwaka mmoja, Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) limeidhinisha Lugha ya Kiswahili kuwa na Siku yake Duniani ambayo ni Julai 7 ya kila mwaka”, amesema Mhe. Mchengrwa.

Waziri Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, hivi karibuni lugha ya Kiswahili imeidhinishwa rasmi na Umoja wa Afrika (AU) kuwa lugha rasmi ya kazi katika umoja huo, akieleza kuwa hatua hiyo itazalisha fursa zaidi za ajira kwa watanzania wenye ujuzi wa Kiswahili na lugha nyingine.

Aidha, katika kipindi hicho cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, imefanikiwa  kuwashirikisha  Machifu kama walinzi wa mila na desturi za watanzania  ili kunufaika na mchango wao, ambapo Mhe Rais aliaahidi kuwa na jukwaa na wazee hao  kila mwaka, huku wizara kwa kushirikiana na  wadau mbalimbali imeanza kuratibu matamasha mbalimbali ya Utamaduni ili kuitangaza nchi  ambapo mwezi Mei mwaka huu 2022, Tamasha kubwa la Utamaduni litakalohusisha makabila na mila chanya za mikoa mbalimbali nchini litafanyika.

Vile vile Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa, Serikali  ya Tanzania ilikasimiwa jukumu la kusimamia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ili kuhifadhi kumbukumbu na historia tukufu ya ukombozi wa bara hilo iliyopo nchini ambapo  katika mwaka mmoja wa  Serikali ya Awamu ya Sita  takribani shilingi bilioni 1.16 zitatumika  kukarabati jengo la iliyokuwa Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika lililopo Dar es Salaam, lengo ni  kulirasimisha kuwa Makao Makuu ya Programu ya Ukombozi wa Bara la Afrika na makumbusho ya historia hiyo adhimu na mchango wa nchi yetu.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwasilisha taarifa ya Mafanikio ya wizara chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Machi 16, 2022 Mtumba jijini Dodoma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi