Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sheria ya Takwimu Haiwabani Wadau bali Inawafungulia Milango Zaidi
May 01, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mwandishi Wetu

Serikali imesisisitiza kuwa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 haiwazuii wadau kukusanya na kusambaza takwimu bali inawataka kufuata vigezo na masharti yaliyowekwa kulingana na sheria hiyo.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari hivi karibuni mjini Kigoma, Mkurugnezi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa alieleza kuwa sheria hiyo badala ya kudaiwa ‘kuwabana’ wadau badala inafungua milango zaidi kwa wadau wenye uwezo na taaluma ya kukusanya takwimu ili kusaidia upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.

“Sheria inawatambua wadau wote katika mfumo wa takwimu ambao wana uwezo wa kukusanya na kusambaza takwimu muhimu ni kwa wadau hao kufuata masharti ya yaliyowekwa” Dk. Chuwa alisema.

Alibanisha kuwa milango ya ofisi yake iko wazi kwa watu wote binafsi au taasisi zinazotaka kukusanya takwimu kushirikiana nao ili kuiwezesha nchi kupata takwimu rasmi kusaidia maendeleo ya nchi.

“NBS haina uwezo wa kuzalisha takwimu zote rasmi zinazohitajiwa na nchi yetu ndio maana inahimiza watu na taasisi kushiriki katika uzalishaji wa takwimu rasmi na kwamba kufanya hivyo kutarahisisha nchi kupata takwimu sahihi na bora” Mkurugenzi Mkuu huyo aliongeza.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari ambao aliufanya mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la ofisi ya NBS mkoani humo, Dk. Chuwa alibainisha kuwa matukio ya upotoshaji wa takwimu rasmi yamepungua tangu Bunge lilipopitisha sheria hiyo mwaka 2015 ambapo imeainisha makossa na adhabu kwa wanaovunja sheria hiyo.

“Takwimu ni suala nyeti ndio maana sheria yetu haivulimii hata kidogo vitendo vya upotoshaji wa takwimu za nchi na hii si hapa kwetu tu ni nchi zote duniani” alisema Dk. Chuwa.

Alibanisha kuwa haiwezekani kwa mfano Serikali imetoa Matokeo ya Viashiria ya Malaria kwa Mwaka 2017 na kuonesha kiwango kimepungua kwa asilimia 7.3 halafu mtu mwingine alete takwimu tofauti.

“Tumeshirikiana na mashirika na wataalamu mbalimbali na tumefuata masharti yote yanayotakiwa hadi kupata takwimu hizi na wenzetu wamelitambua hilo halafu kufumba na kufumbua atokee mtu na ‘vitakwimu vyake’; hiyo haitavuliwa” Alisisitiza Mkurugenzi Mkuu huyo.

Kuhusu jengo la ofisi yake linaloendelea kujengwa alisema uamuzi wa kujenga jengo hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga miunduombinu ya ukusanyaji na usambazaji wa takwimu nchini.

“Kazi za NBS mkoa ni kuratibu takwimu za mikoa hivyo hatuna budi kupanua wigo wa utendaji kazi kwa kutoa huduma hiyo kwa halmashauri zote zilizo mkoni humu” Dk. Chuwa alisema na kusisitiza kuwa jengo hilo litatoa fursa kwa watumishi wa NBS kufanya kazi katika mazingira bora zaidi.

Jengo hilo la ghorofa mbili litakua na vyumba vya ofisi vya kutosha na ukumbi wa mikutano ambao unaweza kutumika na ofisi na taasisi nyingine za Serikali ili kupunguza gharama za kukodi kumbi binafsi.

NBS ina ofisi kila mkoa Tanzania Bara ambazo zinazongozwa na Mameneja wa Takwimu Mkoa ambapo nyingi zao zimo katika majengo ya ofisi za wakuu wa mikoa. Jengo hilo ambalo limefikia hatua ya umaliziaji linatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2020.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi