Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yawahakikishia Soko Wakulima wa Korosho
Nov 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Jacquiline Mrisho

Serikali imewahakikishia wakulima wa korosho kupata soko la uhakika kwa kuendelea kuzungumza na nchi mbalimbali juu ya ununuzi wa zao hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Maftaha Nachuma lililohoji juu ya kauli ya Serikali kuhusu uuzaji wa zao hilo.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali iliweka utaratibu wa minada ambao unawafanya wafanyabiashara kununua mazao kwa namna ya ushindani hali ambayo inawawezesha wakulima wa korosho kuuza kwa bei nzuri hivyo hadi sasa minada imeendeshwa na inaendelea kuendeshwa katika kila Chama Kikuu cha Ushirika ili kuhakikisha zao hilo linapata soko lenye tija.

"Natoa rai kwa wakulima na wadau wa zao la korosho kuendelea kuwa wastahimilivu wakati Serikali inaendelea kutafuta masoko ya zao hilo, kwa sasa tunaendelea kuzungumza na mataifa moja kwa moja ili kupata masoko ya uhakika," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumza kuhusu upatikanaji wa pembejeo kwa bei nafuu, Waziri Mkuu amesema kuwa wizara husika inaendelea na mkakati wake wa kuagiza pembejeo hizo kwa pamoja ambapo mkakati huo umesaidia pembejeo kupatikana kwa bei ya chini karibu asilimia 40 ya bei ya awali.

Waziri Mkuu amefafanua kuwa hadi sasa Serikali imeshaleta mbolea zaidi ya tani 260,000 ambazo tani hizo zinakaribia asilimia 60 ya mahitaji ya nchi na kwa sasa wizara husika inasimamia kupeleka mbolea kwenye maeneo husika mapema angalau mwezi mmoja kabla ya msimu wa zao husika.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali imejipanga kujenga viwanda viwili vya uzalishaji wa mbolea katika Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Kilwa pia Serikali imeendelea kutoa wito juu ya ujenzi wa viwanda hivyo ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbolea. 

Amefafanua juu ya mazingira mazuri kwa wanaohitaji kuwekeza katika ujenzi wa viwanda hivyo kuwa Serikali imetoa ardhi na motisha mbalimbali pamoja na ushirikiano wa Serikali za mikoa ambapo ujenzi wa viwanda hivyo utafanyika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi