Na Grace Semfuko, MAELEZO
Serikali imetangaza msamaha wa riba kwa Waajiri wote katika Sekta ya Umma na Binafsi waliochelewesha kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao ulianzishwa kwa lengo la kushughulikia fidia kwa wafanyakazi watakaoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.
Msamaha huo ni wa riba iliyotozwa kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Oktoba, 2017 hadi tarehe 31 Agosti, 2021 kwa Waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango hiyo.
Mfuko huo unawataka Waajiri wote Tanzania Bara kujisajili na kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila mwezi, ambapo viwango vinavyopaswa kuchangiwa ni asilimia 0.5 ya mshahara ghafi kwa mwezi kwa sekta ya Umma na asilimia 0.6 ya mshahara ghafi katika sekta binafsi, michango ambao huwekezwa na mfuko kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kutoa fidia hizo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akitoa msamaha huo leo Mei 05, 2022, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema lengo ni kuongeza kiwango cha utekelezaji wa hiyari wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi pamoja na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na kuwaondolea waajiri malimbikizo ya madeni.
Serikali haipendi kuona mwekezaji anakwama na biashara yake inafungwa, maelekezo ya Mhe. Rais ni kwetu sisi watendaji kuchambua vikwazo vinavyoonekana kutishia biashara na tunachukua hatua stahiki, tangu Julai 2015 hadi kufikia mwezi Agosti mwaka 2021, michango iliyocheleweshwa ilikuwa inatozwa riba ya asilimia 10 kwa mwezi, na kuanzia Septemba, 2021 riba hiyo imeshushwa kutoka asilimia kumi hadi asilimia 2 kwa mwezi” alisema Waziri Ndalichako.
Alifafanua kuwa Waajiri watakaonufaika na msamaha huo ni wale waliokwishalipa malimbikizo ya michango wanayodaiwa na mfuko wa fidia kwa wafanyakazi na wamebakiza deni la riba pekee.
"Kwa Mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 75 kifungu kidogo cha tano cha sheria ya fidia kwa wafanya kazi sura ya 263, Mimi Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, natangaza msamaha wa riba iliyotozwa kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Oktoba 2017 hadi tarehe 31 Agosti 2021 kwa waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kipindi hicho” alisema Waziri Ndalichako.
Alisema hadi kufikia Agosti 2021, waajiri 13,468 wa sekta binafsi na waajiri 191 wa sekta ya umma walikuwa kwenye orodha ya madeni ya riba.
Alisema waajiri wote watakaolipa malimbikizo ya michango ya miezi ya nyuma wanayodaiwa na mfuko kabla ya juni 30 mwaka huu wa 2022, nao pia watanufaika na msamaha huo wa ondoleo la riba ya michango hiyo na kuongeza kuwa waajiri wote ambao mpaka sasa hawajajisajili kwenye mfuko wa fidia kwa wafanyakazi, watakapojisajili na kulipa michango stahiki inayodaiwa kabla ya juni 30 mwaka huu, naoi a watanufaika na msahama wa riba ya malimbikizo ya madeni ya michango hiyo.
Aidha, Waziri Ndalichako aliwataka waajiri kutumia vizuri msamaha huo uliotolewa na Serikali unaolenga kuongeza kiwango cha utekelezaji wa hiari wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi sura ya 263 katika kuhakikisha waajiri wote wanajisajili katika mfuko na kulipa malimbikizo ya michango ya nyuma bila kutozwa riba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema punguzo hilo la riba litasaidia waajiri kutekeleza wajibu wao wa kuwasilisha malimbikizo ya michango ya wafanyakazi na kuwahamasisha waajiri kuitikia kwa hiyari.
"Tunaishukuru sana Serikali kwa uamuzi huu, ni matumaini yetu waajiri watawasilisha michango yao kwa wakati kwani hii ni hatua muhimu sana” alisema Dkt. Mduma.