Na. Immaculate Makilika. Serikali imetoa asilimia mia moja ya fedha za bajeti ya dawa kwa mwaka 2016/2017 kwa ajili ya manunuzi ya dawa ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha sekta ya afya nchini. Akizungumza katika mahojiano ya kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO na kurushwa na kituo cha televisheni cha TBC, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa, Laurean Bwanakunu alisema kuwa Serikali inawahakikishia wananchi kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 zipo fedha za kutosha ili kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya. “Ikiwa ni asilimia 81 ya upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba katika maeneo ya mjini na vijijini, ambapo Bohari Kuu ya Dawa inahudumia vituo 5642 nchini kote” alisema Bwanakunu. Pia, Bwanakunu alibainisha kuwa hivi sasa kumekuwepo na upatikanaji wa dawa muhimu 110 kati ya 135 katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma za huduma za afya. Katika kuboresha huduma za usambazaji wa dawa nchini , Bohari Kuu ya Dawa imefanikiwa kufungua maduka ya dawa 7 katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Geita, Mbeya na Lindi, ambapo imeanza kusafirisha dawa kwa kutumia ndege na treni ili kufikisha dawa kwa wakati katika vituo mbalimbali vya afya nchini. Aidha, Mikoa na Halmashauri zimetakiwa kuwasilisha maombi yao ya dawa kwa wakati ili kutatua changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. |