Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatoa Bilioni 6.3 Kukarabati Vivuko Nchini
Oct 04, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na. Alfred Mgweno (TEMESA MTWARA)

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, chini ya Wakala wa Ufundi naUmeme Tanzania (TEMESA) imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 6.3 kwamwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa ajili ya kuvifanyia ukarabati mkubwa vivuko nchini ambavyo vimefikia muda wake wa ukarabati.

Hayo yamebainishwa leo wakati wa mapokezi ya kivuko cha MV. MAFANIKIO kilichorejea kutoa huduma mkoani Mtwara baada ya kukamilika kwa ukarabati wake uliochukua takribani miezi miwili na nusu.

Akizunguma na wananchi waliofika kushuhudia tukio la upokeaji wa kivuko hicho lililofanyika katika eneo la Msemo Shangani Mjini Mtwara katika kivuko cha Msangamkuu - Msemo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali, Marco Elisha Gaguti amesema ni utaratibu wa kawaida kwa Serikali kuvifanyia vivuko ukarabati kila inapopita miaka minne hadi mitano ili kuviwezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na hivyo kivuko cha MV. MAFANIKIO wakati wake wa kufanyiwa ukarabati mkubwa ulifikia na hivyo ikawalazimu TEMESA kukiondoa ili kirejee kikiwa kiko salama na tayari kutoa huduma za kubeba abiria na mizigo.

‘’wote tunafahamu kati ya Msangamkuu na Msemo ni takribani mita 700, kwa kivuko hiki tunatumia dakika takribani tano mpaka kumi, lakini ukiondoa kivuko hiki barabara ni kilometa 29, barabara ya changarawe kutoka hapa mpaka Msangamkuu na unatumia zaidi ya saa moja mpaka saa moja na nusu kwa barabara kwa hiyo mnaweza kuona ni kiasi gani kupatikana kwa kivuko hiki baada ya matengenezo makubwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wetu wa Msangamkuu katika swala la usafiri na usafirishaji’’. Alisema Mkuu wa Mkoa ambapo alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha ukarabati huo.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mhandisi Japhet Y. Maselle, akizungumza katika hafla hiyo fupi amesema ukarabati wa kivuko cha MV. MAFANIKIO umefanywa na kampuni ya M/s Songoro Marine Transport Ltd. Boat Yard ya jijini Mwanza kwa gharama ya TZS. 493,609,357.70 (pamoja na ongezeko la kodi-VAT).

‘’Baadhi ya kazi zilizofanyika katika ukarabati huu ni pamoja na Kuweka deki mpya ya magari, kuweka milango mipya miwili (2-New ferry ramps), kuweka ramp lifting cylinder cover mpya, kutengeneza mifumo ya steering, propulsion pamoja na injini na kupaka rangi kivuko chote.’’ Alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa Gharama zote za ukarabati wa kivuko hiki zimegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhandisi Maselle amevitaja vivuko vitkavyofanyiwa ukarabati kwa mwaka huuwa fedha wa 2021/2022 kuwa ni MV. Kitunda (Lindi), MV Tanga (PanganiTanga), MV Kazi na MV magogoni (Dar es salaam), MV Ruhuhu (Ruvuma) pamoja na vivuko vinavyofanya kazi kwenye ziwa Victoria ambapo amesema serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya ukarabati wa vivuko hivyo.

Aidha, Mhandisi Maselle pia ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuendelea kuuamini Wakala na kuahidi kuendelea kutunza kivuko hicho pamoja na vivuko vingine kwa kuvifanyia matengenezo kama inavyotakiwa ili viweze kudumu na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kivuko cha MV. MAFANIKIO kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari sita sawa na tani 50 na kinatoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi