Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatenga Bilioni 20 Kilimo cha Alizeti na Mchikichi
Jun 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuzindua rasmi Vitendea kazi vya uendelezaji wa kilimo katika Mashamba ya Miwa yaliyopo kwenye Kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar mkoani  Kagera tarehe 09 Juni, 2022.

Na Lilian Lundo - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita imetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuyaendeleza mashamba makubwa kwa kupanda Alizeti na Mchikichi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo, Juni 9, 2022 alipotembelea kiwanda cha Sukari Kagera, kilichopo mkoani Kagera, ambapo yupo mkoani humo kwa ziara ya siku tatu iliyoanza Juni 8, 2022.

"Tumekuja na sera ya kilimo cha mashamba makubwa, tumetenga shilingi bilioni 20 kuyaendeleza mashamba makubwa ambapo yatapandwa mbegu za kisasa za Alizeti na Mchikichi ili tuweze kujitosheleza mafuta ndani ya nchi na ikiwezekana tupeleke nje ya nchi,' alisema Rais Samia.

Aliendelea kusema kuwa, moja ya mikoa ambayo imechaguliwa kwa ajili ya kilimo hicho ni Kagera. Hivyo amewaagiza Wakuu wa mikoa na viongozi wa mkoa huo  kuyatambua maeneo ambayo hayana kazi ili yaweze kuendelezwa kwa ajili ya kilimo cha Alizeti na Mchikichi.

Aidha, amesema kuwa, kwa mkoa wa Kagera zitahitajika Heka 70,000 hadi 100,000 za mashamba makubwa ambapo vijana watalima Alizeti na Mchikichi. Vilevile viwanda vitajengwa mkoani humo ili kunyanyua uchumi wa mkoa.

Kwa upande wake, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa, katika kuziba pengo la uzalishaji wa sukari nchini wizara hiyo imekuwa ikihamasisha viwanda vilivyopo kupanua zaidi uwezo wake wa uzalishaji.

"Viwanda vya sukari vya ndani vinauwezo uliosimikwa wa kuzalisha tani 462,863 za sukari kwa mwaka. Aidha, kwa mwaka 2021/2022 viwanda hivyo vilijiwekea lengo la kuzalisha tani 394,606 za sukari, ambapo hadi kufikia Mei, 2022 vimeweza kuzalisha tani 306,871 sawa na asilimia 77 ya lengo walilojiwekea," alisema Dkt. Kijaji

Aidha, amesema kuwa mahitaji ya sukari ndani ya Taifa ni tani 490,000 kwa mwaka ambapo kwa mwezi mmoja zinatumika tani 35,000. Hivyo pengo la sukari mpaka sasa ni tani 42,000 kwa mwaka.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi