Serikali imeendelea kuhakikisha anga ya mtandao nchini inakuwa imara kwa kufanya jitihada za makusudi ambazo zimekuwa msingi ulioifanya Tanzania kuwa miongoni mwa vinara wa usalama mtandao duniani kwa mujibu wa ripoti ya “Global Cybersecurity Index” ya mwaka 2024 inayofanywa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kila baada ya miaka minne.
Jitihada zinazoendelea kufanyika ni pamoja na utungwaji wa sheria mbalimbali zinazoongoza matumizi na usalama wa anga ya mtandao pamoja na uandaaji wa mikakati na mipango madhubuti ya kulinda anga hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu (DAHRM) wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Salome Kessy ameyasema hayo leo Novemba 07, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya usalama wa mtandao kwa watumishi wa wizara hiyo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Bi. Salome amesema kuwa anga ya mtandao haitambui mipaka ya kijiografia hivyo, suala la uhalifu wa mtandao limekuwa ni ajenda ya kikanda na kimataifa ambapo jitihada za mashirikiano ya kuimarisha usalama mtandaoni zimefanyika hususan katika miongozo ya utungwaji wa sheria za usalama mtandaoni na kujenga uwezo wa wataalam katika kukabiliana na uhalifu mtandaoni.
"Pamoja na athari chanya za kukua kwa TEHAMA, kumekuwa na athari hasi za kuongezeka kwa matukio ya uhalifu mtandaoni, hivyo kuilazimu Serikali kuchukua jitihada za makusudi za kuhakikisha anga ya mtandao ya nchi inakuwa salama kwa watumiaji ikiwemo uwepo wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015; Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015; na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022", amesema Bi. Salome.
Amefafanua kuwa, ili kuwalinda watumiaji wa mtandao, ni muhimu kuwajengea uelewa wa namna ya kuwa na matumizi salama ya huduma na bidhaa za TEHAMA ambapo katika jitihada za kuwalinda watumiaji wa mtandao, Wizara kwa kushirikiana na wadau muhimu imetoa elimu ya usalama mtandao kwa watumishi ili kujenga uelewa kuhusu namna wanavyoweza kubaini mashambulizi ya mtandao na kujikinga dhidi ya uhalifu wa mtandao.
Watumishi hao wamepata fursa ya kupewa mafunzo juu ya usalama mtandaoni na wawezeshaji kutoka Jeshi la Polisi Tanzania; AFICTA; na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum ambaye alizungumzia namna bora ya kumlinda mtoto mtandaoni.
Sambamba na mafunzo hayo, watumishi hao walipata mafunzo ya kukumbushwa juu ya matumizi ya Mfumo wa Utumishi Portal katika moduli za Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma (PEPMIS) pamoja na moduli ya e- Uhamisho na e- Likizo yaliyotolewa na wawezeshaji kutoka kutoka Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.