Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yapeleka Neema Msomera
Jan 17, 2024
Serikali Yapeleka Neema Msomera
Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi akizungumza wakati wa mkutano na Wandishi wa Habari uliofanyika leo Januari 17, 2024 katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni.
Na Mwandishi Wetu

Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu na huduma za jamii katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga ili kuwapa fursa wakazi wanaohamia katika eneo hilo kutoka eneo la hifadhi ya Ngororongo mkoani Arusha kuwa na maisha bora kama walivyo Watanzania wengine katika maeneo mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi wakati wa mkutano na Wandishi wa Habari uliofanyika leo Januari 17, 2024 katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni.

Akifafanua, amesema kwa sasa Kijiji hicho kina huduma za mawasiliano ya simu, posta, shule, kituo cha afya, zahanati, mnada, mabwawa, maeneo ya kunyweshea mifugo na visima vya kisasa vya maji na Kituo cha Polisi.

Akieleza kuhusu faida wanazopata wakazi hao, Bw. Matinyi amesema kuwa ni pamoja na uhuru wa kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, kukuza ufugaji ikilinganishwa na Ngororongo ambapo walikuwa hawawezi kufanya hivyo.

Aidha, amesema kuwa wananchi hao wanapewa bure nyumba ya kuishi yenye vyumba vitatu, hekari mbili na nusu za shamba, eneo la malisho ekari tano, kufidiwa mali zao zote na fedha taslimu milioni 10 kwa wanaohamia Msomera.

Sanjari na hilo kwa wanaohamia maeneo mengine nje ya yale yaliyopangwa na Serikali  wanafidiwa mali zao na kupewa shilingi milioni 15 ili kuwawezesha kuanza maisha mapya.

Kuhusu awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 5,000, Bw. Matinyi amesema mradi huo unaendelea kutekelezwa vizuri na utakamilika kama ulivyopangwa ili kuwawezesha wananchi wote wanaohama kwa hiari kupata makazi bora.

Mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali na Waandishi wa Habari ni sehemu ya ziara ya Waandishi hao iliyofanyika kuanzia Januari 14 hadi 17, 2024 katika eneo la Ngororongo na Msomera.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi