[caption id="attachment_1599" align="alignnone" width="750"] Mkuu wa Kitengo cha Dharura Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga akizungumza na Mzee Francis Maige Mara baada ya kupandishwa kwenye gari la kubebea wagonjwa tayari kwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam.[/caption]
Na Benjamin Sawe
Serikali inaendelea na kumpatia matibabu Mzee Francis Maige maarufu kama Ngosha wa Buguruni Malapa Jijini Dar es Salaam ambaye amelazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Mzee Maige ambaye ndiye aliyebuni nembo ya Taifa, alikimbizwa katika hospitali ya Muhimbili akitoke hospitali ya Rufaa ya Amana ya Ilala jijini Dar es Salaam ambapo vipimo vya awali vilionesha kuwa alikuwa akiishiwa nguvu na kupungukiwa damu.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo hii katika hospitali ya Rufaa ya Amana Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema serikali ilisikia juu ya kulazwa kwa Mzee Maige na hivyo kuchukua hatua za haraka kumpeleka Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
“Serikali tulipata taarifa za kuumwa kwa Mzee Maige na ndio maana tumechukua hatua za haraka kumhamishia Muhimbili kwa matibabu na uchunguzi zaidi kwani amekuwa na mchango mkubwa sana na ataendelea kukumbukwa na vizazi vyote nchini kutokana na kazi ya ubinifu aliyoifanya kwa Taifa”, alieleza Naibu Waziri.
[caption id="attachment_1592" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kingwangalla akimjulia hali Mzee Francis Maige Ngosha aliyelazwa kwenye wodi ya Wanaume Hospitali ya Rufaa Amana kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo jijini Dar es Salaam.[/caption]Dkt. Kigwangalla ameelezwa kuwa kwa sasa serikali inashughulikia suala la matibabu na baada ya matibabu na kupona serikali itamtafutia makazi ya kuishi ama kumpeleka katika nyumba ya wazee wasiojiweza iliyopo Nunge Kigamboni.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga alisema kuwa hali ya Mzee Maige inaendelea vizuri lakini amechukuliwa vipimo kwa uchunguzi zaidi.