Na Lilian Lundo – MAELEZO
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika mwaka huu wa fedha, imetoa jumla ya shilingi bil. 9 ikiwa ni fedha za maendeleo kwa shirika la Nyumbu (Tanzania Automotive Technology Centre – TACT).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika na TACT na Kikosi cha Nyumbu Project, Brig. Gen. Hashim Komba alisema hayo katika hotuba yake kwa Waandishi wa Habari waliotembelea shirika hilo, leo Machi 7, 2022 Kibaha mkoani Pwani.
“Tunamshuru Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo kwa mwaka huu wa fedha, fedha zote zilizoainishwa na Bunge shilingi bilioni 9 zimetolewa, ndio maana tumeweza kununua mashine za kisasa kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za shirika,” alifafanua Brig. Gen. Komba.
Aliendelea kusema kuwa, fedha hizo zimetumika kununua mashine za kisasa ambazo zitawezesha shirika hilo kutengeneza vifaa mbalimbali kwa wingi na kwa ubora zaidi, tofauti na mashine ambazo zilikuwa zikitumika zamani ambazo nyingi zilikuwa za mikono.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa TACT-Nyumbu, Meja Simon Rwegoshora amesema kuwa, ununuzi wa mashine mpya utawezesha shirika hilo kupokea tenda nyingi zaidi, ambapo kwa sasa wameingia mkataba na Shirila la Umeme Tanzania (TANESCO) kutengeneza nguzo za chuma ambazo hazishiki kutu.
“Shirika liliamua kuanzisha mradi wa kutengeneza nguzo za chuma zisizopata kutu kwa ajili ya TANESCO na wateja wengine kama Shirika la Reli kupitia mradi wake wa reli ya kisasa (SGR) pamoja na mashirika ya simu kwa ajili ya kutengeneza minara ya simu,” alifafanua Meja Rwegoshora.
Shirika la nyumbu lilianzishwa mwaka 1977 kutokana na maono ya aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Julius Kambarage Nyerere. Shirika linajishughulisha na uundwaji wa gari la Nyumbu kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kiraia, ambako mpaka sasa jumla ya magari 50 ya Nyumbu yameundwa, uundwaji wa magari ya zimamoto, ambapo kati ya mwaka 1986 hadi 1991 wataalamu wa kituo cha nyumbu walifanikiwa kuunda magari ya zimamoto aina tatu.
Miradi mingine inayotekelezwa na Shirika la Nyumbu ni uzalishaji wa vipuri vya gari moshi (Train), kuunda injini, ukarabati wa pampu za maji, utengenezaji wa mageti ya Ikulu Chamwino, mtambo wa kufyatua tofali, mtambo wa kusindika nyuzi fupi za mkonge kwa ajili ya kuzalisha karatasi maalum, mradi wa kuzalisha gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme pamoja na mitambo, viambato na vipuri kwa ajili ya sekta ya kilimo.