Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yafunga Shule za Awali Hadi Kidato cha Sita kwa Siku 30
Mar 17, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

Kufuatia ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) kuingia nchini, Serikali imezifunga shule za awali hadi kidato cha sita kwa muda wa siku 30 kufuatia kugundulika kwa mgonjwa wa Corona nchini.

Tamko hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akitoa msimamo wa Serikali kuoitia vyombo vya habari kuhusiana ugonjwa huo.

 “Tumefunga shule zote kuanzia za awali hadi kidato cha sita, tumesitisha michezo yote ikiwemo ligi kuu na Serikali imefikia uamuzi huo ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini” alisema Waziri Mkuu

Akitaja hatua mbalimbali ambazo Serikali inaendelea kuchukua ni pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ambayo si ya lazima kufanyika kama vile semina na shughuli mbalimbali za kijamii.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema kuwa Serikali imeendelea kufuatilia abiria wanaoingia nchini kupitia maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani, kwa kuwapima abiria ili kubaini kama wanamaambukizi, sambamba na kuimarisha maabara ili iweze kupima na kutambua endapo kuna maambukizi.

“Tumetenga kambi maalum eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam, kituo cha afya cha Buswelo huko Mwanza, hospitali ya Mawenzi ya mkoani Kilimanjaro pamoja na hospitali za Mnazi mmoja, Zanzibar na Chakechake huko Pemba, ambazo zitatumika kuhudumia wagonjwa wa Corona” alisema Waziri Mkuu.

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu alisema kuwa jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali ni kusitisha shughuli za Mwenge na badala yake fedha hizo shilingi bilioni moja zimeelekezwa Wizara ya Afya ili kuwezesha shughuli mbalimbali zitakazosaidia kupambana na ugonjwa huo na tayari shilingi milioni 500 zimeshakabidhiwa Wizara ya Afya.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa angalizo kwa Wizara ya Afya na wafanyabiashara na kusisitiza: “Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kuthibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa viaa hivyo.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kufuatilia kwa karibu na kufanya uchunguzi kuhusu wageni watakao ingia katika maeneo, na wananchi wametakiwa kutoa taarifa katika namba za bure za 0800110037/0800110124 na 0800110125 pindi watakapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka.

Ugonjwa wa Corona ulioanza Disemba mwaka jana nchini China, umesambaa  zaidi katika nchi 150 duniani, na mgonjwa wa kwanza kugundulika nchini  ni Machi 16 mwaka huu ambaye aliwasili nchini kutoka Ubelgiji

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi