Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yadhihirisha Azma Yake ya Uchumi wa Viwanda
Jun 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_44273" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango akionyesha Mkoba unaowakilisha Bajeti Kuu ya Serikali alipowasili katika viwanja vya Bunge leo jijini Dodoma tayari kwa ajili ya kuwasilisha Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020. Serikali imewasilisha mapendekezo ya shilingi tirilioni 33.11 kwa ajili ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2019/2020. (Picha na: Frank Shija)[/caption]

Na Immaculate Makilika, Jonas Kamaleki

Serikali ya Awamu ya Tano imedhihirisha dhamira yake ya dhati ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kwa kuweka mipango na mikakati ya kuwekeza katika viwanda nchini.

Haya yamedhihirishwa leo Bungeni, Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020, ambayo jumla yake ni shilingi trilioni 33.11.

“Katika kuendeleza azma ya kujenga uchumi wa viwanda, katika mwaka 2019/20 Serikali itajikita kuvutia uwekezaji zaidi kwenye viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini kama vile mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini; kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na ziada kwa ajili ya kuuza nje, pamoja na kuongeza fursa za ajira”, alisema Dkt. Mpango

Aidha amesema kuwa sekta ya kilimo kama vile mazao, uvuvi, mifugo na misitu ni muhimu kwa uendelezaji wa viwanda nchini kwa kuwa sehemu kubwa ya malighafi za viwanda zinatokana na kilimo na kuongeza kuwa katika kuimarisha sekta hii, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) hususan kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo, huduma za ugani, masoko, miundombinu wezeshi na tafiti, ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha zaidi kwenye maeneo wezeshi kwa kilimo na kutoa nafuu za kikodi.

 Vile vile katika bajeti hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha bodi za mazao, kuboresha na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya mazao ili kuviwezesha kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye shughuli mbalimbali za kilimo na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya mazao.

 “Uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji: Bajeti hii imeweka msisitizo mkubwa katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan reli, bandari, nishati, barabara, madaraja, na viwanja vya ndege,”alisema Dkt. Mpango

Serikali itaendelea kupitia na kuimarisha  mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Aidha, Serikali imewahakikishia wafanyabiashara, wawekezaji  na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, itaanza kutekeleza mpangokazi wa kuboresha mazingira ya biashara ( Blueprint for the Regulatory Reforms to improve the Business Environment na kuyafanya kuwa rafiki zaidi na yenye gharama nafuu.

Ili kuvutia biashara na uwekezaji nchini Serikali imependekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato. Marekebisho hayo yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika.

Wakati huo huo, Dkt. Mpango amependekeza kufuta au kupunguza ada na tozo hamsini na nne (54) zinazotozwa na Wizara, Idara na taasisi zinazojitegemea ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Hatua hiyo inalenga kuondoa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji baina ya Wizara, Taasisi na Mamlaka za Udhibiti. Marekebisho hayo yatajumuisha  tozo mbalimbali kama vile Mamlaka ya Dawa (TFDA) tozo za Kushikilia usajili wa dawa za chanjo,  inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150), dawa za mitishamba inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia hamsini (150), vifaa tiba inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia moja (100) na  vitendanishi inayotozwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani mia mbili hamsini (250).

Dkt. Mpango amefafanua kuwa lengo la hatua hizi ni kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji ili kuchochea uzingatiaji wa sheria kwa hiari na kuongeza wigo wa wadau wanautumia huduma za TFDA.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi