Serikali imesema kuwa imeweka kiwango maalumu cha ushuru wa forodha wa Dola za Marekani 500 kwa kila tani moja ya ujazo kwenye mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ili kulinda uzalishaji wa ndani.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kiteto, Mhe. Edward Olelekaita Kisau aliyetaka kujua kauli ya Serikali katika kulinda bei ya zao la alizeti kwa kuongeza kodi kwenye mafuta kutoka nje ya nchi.
Mhe. Chande alisema kuwa, serikali inatoza asilimia 0 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta ya kula yaliyozalishwa nchini kwa kutumia mbegu za mafuta ya kula, ikiwemo mbegu za alizeti ili kuhamasisha uzalishaji.
‘‘Hata hivyo, serikali itaendelea kufanya tathmini ya matokeo ya hatua zilizochukuliwa ili kufanya marekebisho pale itakapoonekana inafaa ”, alisema Mhe. Chande.
Alifafanua kuwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwenye mafuta ya kula kutoka nje ikiwemo mafuta ya alizeti yaliyochakatwa kwa kiwango cha mwisho.