Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaahidi Kukarabati Karakana za Uhandisi SUA
Apr 10, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mariam Mwayela, SUA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kutoajumla ya Tsh. 750 milioni kupitia mradi wa kukuza ujuzi na stadi za kazi (ESPJ) ili kukarabati karakana mbalimbali hasa zile za uhandisi kilimo.

Akizungumza wakati akifungua rasmijjuma la Kumbukizi ya Sokoine Dkt. Leonard Akwilapo amesema kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kina mchango mkubwa katika azma ya kuleta mapinduzi katika Kilimo hivyo ukarabati wa karakana hizo una dhumuni la kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine. 

“Katika siku hii ya kihistoria Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itakiunga mkono Chuo kwa kufanya ukarabati mkubwa wa Karakana ili karakana hizi ziwe bora na ziendane na mwenye jina la Chuo, Hayati Sokoine” alisema Dkt. Akwilapo.

Aidha aliongeza kuwa mada ya kumbukizi hili imejikita vyema katika mipangoya sasa ya serikali ya Awamu ya tano hususani dhana kuu tatu ambazo ni uzalishaji katika kilimo, mageuzi ya viwanda na maendeleo ya Tanzania na hivyo kuwataka wanataaluma kufanya uwasilishaji na mijadala mizuri ya maandiko katika mkutano wa kisayansi ili kuwa na mipango mizuri kwa mustakabali wa baadaye kwa kuangalia matokeo ya maadhimisho ya mwaka huu ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine.

Naye Makamu wa Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda alisema kuwa kumbukizi hili limekuwa ni chachu ya kuendeleza mambo mazuri aliyoyafanya Sokoine na kuhakikisha maono yake yanakuwa hai.

“SUA imekuwa ikifanya kumbukizi hili ikiwa ni kama sehemu ya kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine kwa kuendeleza mambo aliyoyafanya na kufanya maono yake kuwa hai kwa ajili ya maendeleo ya Taifa”, alisema Prof. Chibunda.

Prof. Chibunda alisema pamoja na maonesho ya kazi za SUA pamoja na teknolojia pia kutakuwa na mdahalo wa kitaifa ambapo maarifa yatakayopatikana yatahaririwa kwa umahiri na umakini mkubwa na kuchapishwa kwenye toleo maalumu la Jarida la Kisayansi.

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 7 Mei, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli alitembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na kutoa matrekta 10 kwaajili ya mafunzo kwa vitendo ya wanafunzi na wananchi kwa ujumla. Hivyo basi ujio huu wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na ahadi aliyoitoa inaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutekeleza Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 yenye lengo la kuifanya sekta ya kilimo kuwa yenye ufanisi, ushindani na yenye kuleta faida ambayo itachangia kuboresha maisha ya Watanzania na hivyo kufikia uchumi mkubwa na kupunguza umasikini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi