Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaagiza Mikoa, Halmashauri Kuajiri Maafisa Habari
May 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu - TANGA

Serikali imeuagiza uongozi wa Mikoa na Halmashauri ambazo hazina Maafisa Habari/Mawasiliano kuhakikisha inawaajiri wataalamu hao ili waweze kuiunganisha Serikali na wananchi.

Kuajiriwa kwa Maafisa Habari/Mawasiliano kwenye mikoa saba na halmashauri 84 kutatimiza maono ya Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambayo inataka wananchi wapate taarifa kuhusu mambo yanayofanywa na Serikali yao.

“Nimesikia changamoto ya kukosekana kwa Maafisa Habari katika baadhi ya taasisi, mikoa na halmashauri, nafasi zipo kwenye mikoa saba, naagiza Wakuu wa Mikoa waajiri Maafisa Habari/Mawasiliano katika mikoa yao,” ameagiza Waziri Nape.

Agizo hilo limetolewa leo jijini Tanga na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alipofungua kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kitakachoendelea kufanyika hadi Mei 13, 2022.

Pamoja na hilo, Mhe. Waziri Nape amewapongeza Maafisa Habari wanaoisimamia wizara, taasisi au idara za serikali kwa kulitumikia Taifa.

“Nawapongeza Maafisa Habari kwani kuna kazi nzuri imefanyika, natoa rai kwa taasisi zote ziwe na mikakati ya utoaji habari, navishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano wa kutoa taarifa za Serikali,” ameeleza Mhe. Nape.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kwamba maafisa hao wana wajibu wa kulihabarisha Taifa na dunia kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

“Maafisa Mawasiliano wana majukumu yanayohitaji bidii na ubunifu, tunao wajibu wa kulihabarisha Taifa na dunia,” amearifu Dkt. Yonazi.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa amesema kikao hicho hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujengeana uwezo wa namna ya kuisema Serikali kwa ufanisi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi