Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Israel Yaahidi Kupanua Wigo wa Miradi Yao Iliyopo Nchini
Apr 25, 2018
Na Msemaji Mkuu

Serikali ya Israel imeahidi kuendelea kupanua wigo katika miradi yake mbalimbali iliyopo hapa nchini ikiwemo miradi ya afya ili  iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Ahadi hiyo imetolewa jana na  Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Mhe. Aleyet Shaked alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuona ushirikiano uliopo kati ya Taasisi hiyo na Taasisi ya  Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini humo.

Mhe. Shaked alisema kuwa kwa upande wa afya katika Taasisi ya Moyo wamekuwa wakifanya matibabu ya moyo kwa watoto na katika siku za baadaye wataangalia namna ya kuongeza huduma hiyo ili iweze kuwasaidia watu wengi zaidi

“Nikirudi nyumbani nitafanya majadiliano na waziri wa Afya na kumpa  mrejesho wa miradi tunayoifanya hapa nchini, nitamuomba   kuendeleza kukuza uhusiano uliopo kwa kupanua wigo wa miradi yetu  kwenye maeneo mengine ya afya katika  sehemu zingine za nchi hii itasaidia  kuweza kufikia watu wengi zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof.  Mohamed Janabi alisema  kabla ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 asilimia 65 ya upasuaji wa moyo kwa watoto ulikua unafanywa na madaktari wa nje kwa kushirikiana na watanzania.

Hivi sasa  madaktari wa Taasisi hiyo wanafanya upasuaji wa moyo kwa watoto kwa asilimia 70 na asilimia 30 inafanywa  kwa ushirikiano na wageni wanaokuja katika  kambi maalum za matibabu hii ni kutokana na upasuaji mwingine kuhitaji  utaalam wa juu zaidi.

“Tangu tumeanza kufanya kazi kama Taasisi mwaka 2015 hadi sasa tumeshafanya upasuaji wa moyo kwa  watoto 400 na asilimia 70 ya hao watoto wamefanyiwa na daktari wetu bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa watoto Godwin Sharau ambaye amesoma nchini Israel”, alisema  Prof. Janabi.

Mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza ushirikiano na SACH  kwa kusomesha madaktari na wauguzi na kufanya  kambi maalum za matibabu ya moyo kwa watoto ambapo watoto wanaokutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya hali ya juu wanatibiwa nchini Israel bila malipo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi