Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Tano Yajizatiti Kuboresha Elimu Nchini
Oct 06, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_47763" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akitoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wahariri wa Vyombo vya Habari.[/caption]

Na Lilian Lundo, MAELEZO - Dar es Salaam

Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika sekta ya elimu hapa nchini ili kuhakikisha kila Mtanzania anaelimika na kuwa mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Hayo yameelezwa jana, Jumamosi Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa mkutano wa viongozi wa wizara hiyo na wahariri wa vyombo vya habari.

[caption id="attachment_47764" align="aligncenter" width="452"] Wahariri na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mkutano kati yao na viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Jijini Dar es Salaam.[/caption]

"Ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu, Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari tangu mwaka 2016 ambapo wanafunzi wa kwanza wanaonufaika na sera hiyo wanatarajia kumaliza kidato cha nne mwishoni mwa mwaka huu"

Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa katika kuboresha elimu, Serikali imetumia  jumla ya shilingi bilioni 93.8  kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ukarabati wa majengo katika shule 588 za msingi na sekondari zikiwemo shule kongwe.

Vilevile Serikali imeongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 424.7 mwaka 2018/2019 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/2020. Aidha makusanyo ya madeni ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu yameongezeka kutoka shilingi bilioni 21.1 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 183.2 mwaka 2018/2019.

[caption id="attachment_47765" align="aligncenter" width="474"] Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe akitoa neno la shukrani kwa Wahariri wa vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya viongozi wa wizara hiyo na Wahariri wa Vyombo vya Habari, uliofanyika Ofisi za NACTE, Jijini Dar es Salaam.[/caption]

Kwa upande wake Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema utoaji wa elimu msingi bila malipo umechochea hamasa ya Watanzania kushiriki katika elimu, ambapo imepelekea ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi ngazi ya elimu ya awali kutoka wanafunzi 1,069,823 mwaka 2015 hadi wanafunzi 1,424,260 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 33.1.

Dkt. Mtahabwa amesema kuwa, shilingi bilioni 23 hutolewa kila mwezi kwa ajili ya kutekeleza sera ya elimu bila malipo katika shule za serikali za msingi na sekondari.

Aidha, Muwakilishi wa Mkurugenzi wa  Idara ya Elimu ya Ufundi, Fanuel Mshana amesema kuwa mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwa na vyuo vya Elimu ya Ufundi katika kila Kanda, Mikoa na Wilaya.

"Shilingi bilioni 4.93 zimetumika kufanya ukarabati wa vyuo 10 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na ukarabati  huo umekamilika. Vyuo hivyo ni Ileje, Nkasi, Newala, Urambo, Mureba, Kilindi, Nyamidaho, Kanadi, Samunge na Babati, baadhi vimeanza kutoa mafunzo ya muda mfupi," amesema Mshana.

Ameeleza kuwa jumla ya vyuo vya maendeleo ya wananchi 20 vimefanyiwa ukarabati na kuongezewa majengo mapya katika awamu ya I, ambapo jumla ya shilingi bilioni 8.7 zimetumika. Awamu ya II ya ukarabati wa vyuo vya maendeleo ya wananchi umeanza tarehe 15.08.2019 na unatarajia  kukamilika tarehe 31.12.2019. Jumla ya shilingi bilioni 12 zimetengwa katika awamu hii. Awamu ya III ya ukarabati itahusisha vyuo vya maendeleo ya wananchi 14 na inategemewa kuanza mwezi Januari, 2020

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe, amesema, wizara ya elimu iko tayari kufanya kazi na vyombo vya habari kwa kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu sekta ya elimu ili wananchi waweze kupata taarifa zinazohusu sekta hiyo pia kufahamu fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi